Mutharika asisitiza umiliki wa ziwa Malawi
13 Agosti 2014Mutharika aliwaambia waandishi habari mjini Lilongwe siku ya Jumanne kuwa nchi yake haitapigana vita na Tanzania lakini ziwa hilo ni mali ya Malawi kwa zaidi ya miaka 104.
Aliongeza kuwa sheria iko wazi, lakini anafikiri kuna nafasi finyu ya majadiliano kuhusu suala hilo, lakini akadokeza kwamba nchi hizo mbili zinaweza kupata njia ya kutatua tatizo hilo.
Kwa msingi wa makubaliano ya wakoloni mwaka 1890, Malawi inadai udhibiti wa ziwa lote la Malawi, ambalo linaaminika lina hazina ya mafuta na gesi.
Tanzania inasisitiza kuwa nusu ya ziwa hilo iko ndani ya mipaka yake na tayari inaangalia uwezekano wa kufanya utafiti wa gesi ya asili katika ziwa hilo.
Mutharika amesema amekutana na rais wa Tanzania Jakaya Kikwete wakati wa mkutano wa Marekani na mataifa ya Afrika nchini Marekani wiki iliyopita na kumwalika kwenda kuvua katika ziwa hilo.
Rais wa zamani Joyce Banda ambaye ameshindwa na Mutharika katika uchaguzi wa mwezi Mei, amekuwa mara kwa mara akitishia kulipeleka suala hilo katika mahakama ya kimataifa.
Mwandishi: Sekione Kitojo
Mhariri: Josephat Charo