1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Muuaji wa Canada alikuwa na chuki dhidi ya Waislamu - Polisi

8 Juni 2021

Polisi nchini Canada inasema kuwa mshambuliaji aliyewauwa watu wanne wa familia ya Waislamu wenye asili ya Pakistan kwa kuwaponda kwa gari, alifanya hivyo kwa sababu ya chuki zake za kidini.

Weltspiegel 08.06.2021 | Kanada Ontario, London | Angriff auf Muslime
Picha: Carlos Osorio/REUTERS

Ikiwanukuu mashahidi wa tukio hilo, polisi ya mji wa London katika jimbo la Ontario iLIsema kwamba kijana wa miaka 20 aliyetambuliwa kwa jina la Nathaniel Veltman aliliekeza kwa makusudi gari lake kunako familia hiyo ya watu wenye asili ya Pakistan, wa umri wa baina ya miaka 9 na 74 na kisha kutimuwa mbio na gari lake baada ya kuwauwa wanne kati yao.

Mkuu wa upelelezi wa idara ya polisi ya London, Paul Waight, aLIsema kuna ushahidi wa kutosha kwamba tukio hilo la siku ya Jumapili (Juni 6) "lilipangwa, lilidhamiriwa na lilitendwa kwa sababu ya chuki, na kwamba wahanga hao walilengwa kwa sababu ya kuwa kwao Waislamu."

Ingawa polisi hawakuchapisha majina ya wahanga wa mashambulizi hayo, lakini gazeti la London Free Press liliwataja kuwa ni Syed Afzaal mwenye umri wa miaka 46, mkewe Madiha Salman mwenye umri wa miaka 44, na binti yao mwenye umri wa miaka 15, Yumnah Afzaal.

Mama yake Syed Afzaal mwenye umri wa miaka 74 pia aliuawa. Mtu pekee aliyesalimika hadi sasa ni mtoto wao wa kiume mwenye umri wa miaka 9, Faez Afzaal, ambaye kwa sasa anatibiwa hospitalini.

Familia hiyo ilihamia Canada kutoka Pakistan miaka 14 iliyopita.

Mashitaka ya mauaji na ugaidi

Polisi walikamata mshambuliaji huyo akiwa kwenye maegesho ya jengo la maduka mengi bila ya kufanya tabu yoyote, akiwa amevamilia kizibao cha kujikinga na risasi.

Polisi wa London, Canada, wakichunguza eneo la tukio baada ya mauaji ya watu wanne wa familia moja.Picha: Geoff Robins/Zuma/picture alliance

Walimshitaki kwa makosa manne ya mauaji ya kukusudia na moja la kujaribu kuuwa na alitarajiwa kupandishwa kizimbani siku ya Alkhamis.

Mbali na mashitaka haya, polisi ya London, mji ulio umbali wa kilomita 200 kusini magharibi mwa mji mkuu wa Canada, Toronto, walikuwa wanashauriana na polisi ya shirikisho na waendesha mashitaka wa serikali kuu juu ya uwezekano wa kufunguwa mashitaka ya ugaidi.

Kwa mujibu wa polisi, mshambuliaji huyo hana rikodi yoyote ya uhalifu na wala hafahamiki kuwa mwanachama wa kundi lolote lenye chuki dhidi ya jamii nyengine na hawakuwa na ushahidi unaoonesha ikiwa alikuwa na watu alioshirikiana nao kwenye mauaji hayo.

Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau aliyaita mashambulizi hayo kuwa ni "habari za kuogofya", akiongeza kwamba chuki dhidi ya Waislamu hazina nafasi kwenye jamii ya Canada. 

Mashambulizi hayo na mabaya kabisa dhidi ya jamii ya Waislamu nchini Canada tangu mtu mmoja kuwauwa Waislamu sita kwa risasi katika msikiti wa mji wa Quebec mwaka 2017.

Meya wa mji wa London, Ed Holder, alisema mauaji hayo "ni dhidi ya Waislamu na dhidi ya wakaazi wote wa mji wa London."