Muujiza wa Milan! Schalke 04 yaichapa Inter Milan 5-2
6 Aprili 2011Mechi kati ya magwiji hao wawili wa soka ilikuwa ya kusisimua tangu mwanzo, kwani bao la kwanza lilifungwa sekunde ya 25 na mchezaji wa Inter Milan Dejan Stankovic. Katika dakika ya 17, Schalke ilifanikiwa kupata bao la kusawazisha lililofungwa na Joel Matip. Kabla ya kufikia muda wa mapumziko, timu zote mbili ziliongeza bao moja - Diego Milito wa Inter alipachika bao lake dakika ya 34 na Edu wa Schalke katika dakika ya 40.
Katika kipindi cha pili cha mechi hiyo, Schalke iliongeza mabao mawili yaliyofungwa na Raul katika dakika ya 53 na Edu katika dakika ya 75. Andrea Ranocchia wa Inter Milan aliiongeza furaha ya mashabiki wa Schalke, alipojifunga bao mwenyewe. Licha ya kuwa na wachezaji nyota kama Samuel Eto'o, Inter Milan haikuweza kufua dafu mbele ya Schalke.
Mwishoni timu ya kocha mpya wa Schalke 04, Ralf Ragnick iliweza kung'ara mbele ya mashabiki wake katika uwanja wa San Siro, katika mpambano ambao umeelezwa kuwa ni "Muujiza wa Milan".
Mwandishi: Elizabeth Shoo/DPA
Mhariri: Josephat Charo