1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Muungano wa kijeshi kusitisha vita Yemen

15 Novemba 2018

Saudi Arabia inashinikizwa na jumuiya ya kimataifa kusitisha vita Yemen dhidi ya Wahouthi ili kutoa nafasi ya kufanyika mazungumzo ya amani yaliyopangwa kuandaliwa huko Sweden na Umoja wa mataifa

Jemen Hodeida Regierungstruppen rücken vor
Picha: Getty Images/AFP/K. Ziad

Muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia katika vita vya Yemen umeagiza kikosi chake kisimamishe vita dhidi ya waasi wa kihouthi katika mji wa bandari kuu wa Hodeidah. Duru tatu zimethibitisha taarifa hiyo kupitia shirika la habari la Reuters.

Kusitishwa kwa mashambulizi dhidi ya waasi wakihouthi ni hatua iliyochukuliwa na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia katika wakati ambapo washirika wake muhimu wa nchi za Magharibi ikiwemo Marekani wakiushinikiza muungano huo uweke chini silaha kabla ya juhudi za mazungumzo ya amani kuanza yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa.

Juhudi hizo zinalenga kuvimaliza vita vya zaidi ya miaka mitatu ambavyo vimezidi kuisogeza Yemen katika janga kubwa la njaa. Duru za kijeshi zinasema muungano unaoongozwa na Saudi Arabia umetowa maelekezo kwa wanajeshi wake walioko Hodeida kusitisha mapigano katika mji huo.Lakini wakaazi wa mji huo wanamashaka kila uchao. 

Picha: Getty Images/AFP/E. Ahmed

Hata wachambuzi wa mambo wanasema kuna kila uwezekano kwamba muda wowote mashambulizi yakaanza upya.Mkuu wa shirika la mpango wa chakula duniani WFP David Beasley aliyekamilisha ziara ya siku tatu huko Yemen ametowa mwito wa amani ili kuyanusuru maisha ya mamilioni ya watu. Pamoja na duru mbali mbali kuthibitisha kwamba vita vinasitishwa,msemaji wa muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudia hakukubali kutoa jibu mara moja juu ya suala hilo pale alipotakiwa na shirika la habari la Reuters kuzungumzia taarifa hizo.

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa Martin Griffiths anajaribu hivi sasa kuyanusuru mazungumzo kati ya pande zinazovutana katika mgogoro wa Yemen baada ya duru ya mwisho mwezi Septemba kuporomoka kufuatia hatua ya waasi kutoshiriki. Saudi Arabia inashinikizwa na Jumuiya ya Kimataifa kuweka chini silaha na kutoa nafasi kwa mazungumzo hayo.

Ikumbukwe kwamba Nchi hiyo ya Saudi Arabia na Umoja wa falme za kiarabu zilijiingiza kwenye vita vya Yemen 2015 kuirudisha madarakani serikali iliyokuwa ikitambuliwa na jumuiya ya Kimataifa,iliyotimuliwa mjini Sanaa na waasi wa Kihouthi mwaka 2014.

Picha: Getty Images/AFP

Nchi hizo washirika zikitegemea silaha kutoka nchi za Magharibi pamoja na msaada wa kijasusi katika mgogoro unaoangaliwa kama ni vita kati ya serikali ya mjini Riyadh na ile ya Tehran inayowaunga mkono Wahouthi. Rais wa Yemen Abedrabbo Mansouri Hadi ameunga mkono mazungumzo ya Umoja wa Mataifa yatakayofanyika Sweden, ya kumaliza vita lakini pia ameapa kuukombowa mji unaoshikiliwa na waasi wa Hodeida kwa namna yoyote ile.Amesisitiza kwamba mapambano ya watu wa Yemen ya kuukomboa mji huo wa Hodeida hayawezi kuepukika iwe ni kwa njia ya amani au vita.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Iddi Ssessanga

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW