1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Muungano wa kiraia Sudan wakataa kuzungumza na jeshi

11 Novemba 2021

Sudan bado yakabiliwa na mtihani wakati jeshi halitaki kurudisha serikali ya kiraia.Baraza la usalama litaarifiwa kikamilifu juu ya hali ya nchi hiyo katika kikao maalum cha Faragha huko New-York.

Sudan Khartum Proteste gegen Militärputsch
Picha: MOHAMED NURELDIN ABDALLAH/REUTERS

Muungano mkuu wa kisiasa wa kiraia nchini Sudan umekataa kuwa na mazungumzo yoyote na jeshi lililotwaa madaraka kwa nguvu kupitia mapinduzi.

Kwa mara ya kwanza tangu yalipofanyika mapinduzi nchini Sudan, jana Jumatano muungano huo wa kisiasa wa kiraia umefanya mkutano na waandishi habari na kuweka wazi msimamo wake.Msemaji wa muungano huo Alwathiq Elbereir aliisoma taarifa yao mbele ya mkutano huo akieleza kile wanachokiamini.

 "Tunasisitiza  hatutokutana na jeshi na msimamo wetu uko wazi kabisa,hakutokuweko mazungumzo yoyote na hatutoshirikiana na waliofanya mapinduzi.Tunauunga mkono msimamo imara uliochukuliwa na waziri mkuu Abdallah Hamdok''

Taarifa hiyo bila shaka imeweka wazi kwamba muungano wa kiraia wa kupigania  uhuru na mabadiliko FFC uliotia saini makubaliano ya kugawana madaraka na jeshi  mnamo mwaka 2019 baada ya kuondolewa kwa nguvu Omar al Bashir unayapinga kwa dhati mapinduzi yaliyofanywa na jeshi na hautaki kabisa kukutana na jeshi hilo.

Picha: /AP/dpa/picture alliance

Muungano huo umesema unamunga mkono waziri mkuu Abdalla Hamdok ambaye hadi sasa yuko chini ya kifungo cha nyumbani lakini bado hawajakutana nae kuungana pamoja kudai kurudishwa kwa mfumo wa katiba uliokuweko kabla ya mapinduzi.

Aidha msemaji wa muungano huo wa FFC amesisitiza pia kwamba muungano huo hautokubali mkuu wa majeshi  jenerali Burhani kurudi kwenye nafasi ya uongozi wa nchi aliyokuwa akiishikilia kabla ya kufanya mapinduzi. Msemaji huyo pia ameongeza kusema kwamba mapinduzi yaliyofanywa hayaiwakilishi taaisisi ya jeshi. Juhudi za mazungumzo tangu jeshi kutwaa madaraka,zimekwama na jeshi limefanya uteuzi kadhaa mdogo lakini limeshindwa kufanya uteuzi wowote wa wakuu wa baraza la uongozi wala mawaziri.

Picha: Loey Felipe/Xinhua/picture alliance

Jenerali Burhani anakabiliwa na shinikizo kubwa kutoka jumuiya ya kimataifa ya kumtaka abadilishe mwelekeo na kuirudisha madarakani serikali ya kiraia. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litapewa taarifa kuhusu Sudan na mjumbe wake maalum wa nchi hiyo Volker Perthes katika mkutano wa faragha utakaofanyika leo alhamisi.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW