1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Muungano wa wahafidhina wa Merkel unaweza kun'golewa

3 Aprili 2017

Uchunguzi mpya wa maoni Ujerumani unaonyesha chama (SPD) kinaweza kuunda serikali ya mseto kwa kushirikiana na chama cha Mazingira na kile cha mrengo wa kushoto Di Linke iwapo uchaguzi utafanyika hivi karibuni Ujerumani.

Symbolbild Rot-Rot-Grüne Koalition
Picha: Imago/C. Ohde

Gazeti la "Bild am Sonntag" limeripoti Jumapili kwamba kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni Chama hicho cha SPD kimeupiku tena muungano wa wahafidhina wa chama cha Angela Merkel cha Christian Demokrat(CDU) na chama ndugu cha Christian Social Union (CSU).

"Sonntagstrend" uchunguzi wa maoni uliofanywa na asasi ya kuchunguza maoni ya Emnid umeonyesha chama cha SPD kikiimarika kwa asilimia moja katika kipindi cha wiki moja kufikia asilimia 33 wakati chama cha CDU na chama ndugu cha jimbo la Bavaria CSU vikishuka kwa asilimia moja na kuwa katika kiwango cha asilimia thelathini na mbili.

Matokeo hayo yanaonyesha kwa mara ya kwanza katika baada ya kipindi cha miaka kumi chama hicho cha mrengo wa wastani kushoto SPD kimevipiku vyama hivyo vya kihafidhina katika uchunguzi wa maoni wa "Sonntagstrend" ambao asasi ya Emnid imekuwa ikiufanya kila wiki kwa ajili ya gazeti la "Bild a Sonntag".

Uchunguzi mwengine wa maoni wa hivi karibuni uliofanywa kwa ajili ya gazeti la "Bild"na asasi ya Insa pia umeonyesha chama hicho cha SPD kikiwa mbele ya kundi la vyama vya CDU/CSU kwa mara ya kwanza baada ya kipindi cha muongo mmoja.

Nyekundu-nyekundu-kijani

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na kiongozi wa chama cha SPD Martin Schulz.Picha: picture-alliance/dpa/G. Fischer

Wakati vyama vya "Die Linke " cha sera kali za mrengo wa kushoto na kile cha Mazingira vikiendelea kushikilia asilimia zao nane na saba kila mmoja uchunguzi huo wa maoni unadokeza kwamba muungano wa serikali ya mseto wa vyama vitatu vya mrengo wa kushoto ambao ungeitwa muugano wa rangi  nyekundu-nyekundu -kijani kwa mujibu wa mfumo wa rangi za kisiasa nchini Ujerumani utakuwa na serikali ya viti vingi bungeni iwapo uchaguzi utafanyika katika kipindi cha wiki moja inayokuja.

Mafanikio hayo ya hivi karibuni ya chama cha SPD katika uchunguzi wa maoni umechangiwa kwa kiasi kikubwa na kuchaguliwa kwa spika wa zamani wa bunge la Ulaya Martin Schulz mwenye kipaji kuwa kiongozi wao kuchukuwa nafasi ya Sigmar Gabriel ambaye amejiuzulu kama kiongozi wa chama ili kuwa waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani.

Chama rafiki kwa biashara cha Free Demokratik (FDP) pia kimeendelea kushikilia umashuhuri wake kwa mujibu wa uchunguzi huo wa maoni kwa kujipatia asilimia sita. Lakini chama kinachopinga uhamiaji na chenye mashaka na Umoja wa Ulaya kinachojulikana kama Chama Mbadala kwa Ujerumani (Afd) kimeendelea kuporomoka kwa kupoteza asilimia moja na kufikia ailimia tisa kiwango cha chini kabisa cha umashuhuri wake katika uchunguzi wa maoni katika kipindi cha mwaka mmoja.

Uchaguzi mkuu wa Ujerumani umepangwa kufanyika tarehe 24 Septemba mwaka huu.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/dpa/ DW

Mhariri :Sudi Mnette

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW