Mvua kubwa yasababisha vifo vya watu 36 nchini Brazil
20 Februari 2023Katika taarifa iliyotolewa na serikali ya Brazil, watu 35 wamekufa katika mji wa Sao Sebastiao na msichana wa umri wa miaka 7 kufariki dunia katika mji jirani wa Ubatuba. Miji ya Sao Sebastiao, Ubatuba, Ilhabela na Bertioga, ni baadhi ya miji iliyoathirika zaidi kutokana na mvua hiyo kubwa. Kutokana na hali ya hatari iliyotangazwa kwenye maeneo hayo, sherehe muhimu za kanivali zimefutwa huku makundi ya waokoaji yakihangaika kuwatafuta waliopotea, waliojeruhiwa na waliopoteza maisha kwenye matope.
Waokoaji washindwa kufikia maeneo
Meya wa Sao Sebastiao, Felipe Augusto, amesema kuwa makundi hayo ya waokoaji yanashindwa kufikia maeneo mengi na kwamba hali ni tata. Augusto ameongeza kuwa kuna mamia ya watu waliopotea na kwamba nyumba 50 ziliporomoka mjini humo kutokana na maporomoko ya ardhi. Augusto alichapisha video kadhaa katika mitandao ya kijamii zilizoonesha uharibifu mkubwa mjini humo pamoja na video ya mtoto aliyekuwa akiokolewa na wakazi wa eneo hilo waliokuwa wamejipanga katika barabara zilizofurika mjini humo. Kupitia ujumbe katika mtandao wa twitter, rais wa nchi hiyo, Luiz Inacio Lula da Silva, amesema atazuru eneo hilo (Jumatatu 20.02.2023).
Katika taarifa yake, serikali ya jimbo la Sao Paulo imesema kuwa mvua hiyo ilipita kiwango cha milimita 600 kwa siku moja, hiki kikiwa kiwango cha juu zaidi kuwahi kutokea nchini Brazili katika kipindi kifupi kama hicho. Serikali hiyo imeendelea kusema kwamba katika mji wa Bertioga pekee, kulikuwa na mvua ya kiasi cha milimita 687 wakati wa kipindi hicho. Gavana wa eneo hilo, Tarcisio de Freitas, alisema kuwa ameomba msaada wa jeshi ambalo lilituma ndege mbili na makundi ya uokoaji katika eneo hilo. Picha za televisheni zilionesha nyumba zilizofurika maji huku mapaa pekee yakionekana. Wakaazi wanatumia mashua ndogo ndogo kubeba bidhaa na kuwahamishia watu katika maeneo ya juu. Barabara inyaounganisha mji wa Rio de Janeiro kuelekea katika mji wa bandari wa Santos ilifungwa kutokana na maporomoko na mafuriko.
Mvua zaidi yatarajiwa kunyesha
Utabiri wa hali ya hewa unaonesha mvua kubwa itaendelea katika eneo la pwani la Sao Paulo, hali inayokwambisha juhudi za timu za ulinzi wa raia na idara ya zimamoto na kuongeza wasiwasi ya idadi kubwa ya vifo. Serikali ya kuu ya shirikisho pia imezitaka wizara kadhaa kuwasaidia waathiriwa, kurekebisha miundombinu na kuanza kazi ya ujenzi. Jimbo la Sao Paulo limetangaza siku 180 za hali ya hatari kwa miji sita baada ya kile wataalamu walichokitaja kuwa tukio baya lisilo la kawaida.