1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mvua kubwa zatatiza shughuli nyingi jijini Dar es salaam

George Njogopa14 Oktoba 2020

Nchini Tanzania kumezuka mjadala kuhusu ubora wa miundombinu ya barabara pamoja na madaraja baada ya kushuhudia mamia ya watu wakikwama barabarani kwa zaidi ya saa saba hadi tisa kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

Tansania Überschwemmung in Daressalaam
Picha: Said Khamis/DW

Mjadala huo unapata nguvu mpya hasa wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu ambako baadhi ya wagombea wamekuwa wakitoa ahadi za kuboresha miundombinu na kulisuka upya jiji la Dar es Salaam.

Kila kona hadithi ni ile ile moja, jinsi mamia ya watu walivyonasa barabarani wakitumia zaidi ya saa tisa kufika majumbani mwao huku wengine wakisemekana kusitisha safari zao na kulala kwa ndugu na jamaa.

Basi la mwendokasi kama linavyoonekana katikati ya kina cha majiPicha: Said Khamis/DW

Ni kwa mara ya kwanza tangu jiji hilo la kibiashara liwekewe barabara za juu pamoja na kubadilishwa sehemu ya miundombinu yake,  kushuhudia msongamano mkubwa wa magari kiasi hicho, hali ambayo inazidisha wasiwasi juu ya hali itakavyokuwa katika siku za usoni.

Kujaaa kwa maji kwa barabara nyingi pamoja na maeneo mengine, kunaelezwa huenda kumesababisha na ujenzi wa barabara zinazojengwa sasa ambazo zimeshindwa kuweka njia kwa ajili ya maji hayo kupenya na kupita.

Wasiwasi bado ni mkubwa miongoni mwa wakazi wengi wa jiji hilo kuu kibiashara, iwapo kiwango cha mvua kikashuhudiwa tena kitarejea hasa nyakati za usiku.

Ingawa siku ya Jumatano hali ya usafiri imerejea kwenye hali yake ya kawaida, hata hivyo usumbufu uliojitokeza kutokana na mvua hizo bado unaendelea kuwakumbusha mengi wakazi wake. Eneo la Jangwani ndilo linalotajwa kukumbwa na adha hiyo kubwa.

Baadhi ya nyumba zikiwa katikati ya kina cha maji kutokana na mvua Dar es salaamPicha: Said Khamis/DW

Mamlaka ya hali ya hewa imeonya kurejea tena kwa kiwango cha mvua na imewataka wananchi wanaoendelea kuwepo kwenye maeneo hatarishi kama yale yenye maporomoko kuchukua tahadhari.

Kulingana na mchambuzi wa masuala ya hali ya hewa wa mamlaka hiyo, Joyce Mkwata mvua nyingine kubwa inatarajiwa kunyesha tena siku ya Alhamisi, ingawa siyo kubwa sana kama ile ya Jumanne.

Hadi sasa hakuna mamlaka yoyote iliyotoa tathmini kama kumekuwa na uharibifu wowote uliosababishwa na mvua hizo zinazoendelea kunyesha.


 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW