Mvua kubwa na yasababisha vifo vya takriban watu 100 Brazil
17 Februari 2022
Ofisi ya meya wa mji wa Petropolis kufikia sasa, imerekodi vifo 104 huku watu 24 wakiokolewa na maafisa wa zima moto. Mvua hiyo kubwa ilionyesha siku ya Jumanne, ambayo ilizidi kipimo cha wastan cha mwezi mzima wa Februari, ilisababisha maporomoko ya udondo yaliofunika nyumba, mafuriko barabarani na kusombwa kwa magari na mabasi.
Picha zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha mafuriko yakikokota magari na nyumba huku maji yakijaa mjini kote. Moja ya video ilionyesha mabasi mawili yakizama kwenye mto uliokuwa umefurika huku abiria wake wakiruka nje ya mabasi hayo kupitia madirishani kutafuta usalama. Wengine hawakufanikiwa kufikia kingo za mto huo na kusombwa na maji.
Katika mkutano na wanahabari, gavana wa Rio de Janeiro Claudio Castro alisema kwamba mvua hiyo ni mbaya zaidi kunyesha katika mji huo wa Petropolis tangu mwaka 1932 na kwamba hakuna ambaye angetabiri mvua kubwa kama hiyo.
Idara ya utabiri wa hali ya hewa imetabiri mvua zaidi katika siku zilizosalia wiki hii. Castro ameongeza kuwa takriban watu 400 wameachwa bila makao. Rais wa Brazil Jair Bolsonaro ameahidi kulisaidia eneo hilo na kusema atatembelea maeneo yaliathirika siku ya Ijumaa atakaporejea kutoka ziara rasmi nchini Urusi na Hungary
Eneo la hilo la milimani lililoathirika, limeshuhudia majanga kama hayo katika miongo ya hivi karibuni, ikiwa ni pamoja na lile lililosababisha vifo vya zaidi ya watu 900. Tangu miaka hiyo, Petropolis iliwasilisha mpango wa kupunguza hatari zamaporomoko ya ardhi, lakini kazi zimekuwa zikiendelea polepole. Mpango huo uliowasilishwa mwaka 2017, ulizingatia tathmini iliyobainisha kuwa asilimia 18 ya maeneo ya mji huo yalikuwa katika hatari ya maporomoko ya ardhi na mafuriko.
Mamlaka katika eneo hilo inasema zaidi ya wakazi 180 wanaoishi katika maeneo ya hatari kwasasa wamepata makao katika shule. Vifaa zaidi na maafisa wa msaada wanatarajiwa kusaidia katika juhudi za uokoaji Alhamisi 17.02.2022.