Mvutano kuhusu uanachama wa Uturuki katika Umoja wa Ulaya
28 Julai 2010Kubwa,masikini na tata - hayo ni maneno matatu yanayowazwa na mataifa mengi ya Umoja wa Ulaya kuhusiana na Uturuki. Kwa ukubwa, Uturuki inaizidi Ufaransa, na kwa idadi ya umma, ni takriban sawa na Ujerumani na kwa pato la wastani la kila mmoja, ni masikini kuliko Rumania. Na hali ya kutatanisha inayofungamanishwa na ugeni na utamaduni tofauti, ni suala ambalo ni nadra kabisa kutamkwa waziwazi katika Umoja wa Ulaya, lakini hiyo ni fikra inayoibuka kwa mfano, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel anapokariri:
"Naamini kuwa uhusiano wa karibu na ulimwengu wa Kiislamu,hasa Uturuki katika Umoja wa Ulaya ni kwa maslahi yetu wote. Bado tunaendelea kubishana iwapo uhusiano huo utakuwa ushirikiano wa upendeleo au uwanachama kamili."
Hayo alitamka Kansela Merkel mwaka uliopita mjini Prague, baada ya Rais wa Marekani Barack Obama kugusia suala la uanachama wa Uturuki.
Kwa upande mwingine Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy amesema kinagaubaga:
"Siamini kuwa Uturuki ina nafasi katika Umoja wa Ulaya. Katika suala hilo, sikubadili maoni yangu."
Lakini Merkel na Sarkozy, hawawezi kubadili chochote kuwa Umoja wa Ulaya unajadili rasmi uanachama wa Uturuki, kwani katika mwaka 2004 viongozi wa umoja huo walikubaliana kwa kauli moja kuanzisha majadiliano hayo. Baada ya wanachama 12 wapya kupokewa kwenye Umoja wa Ulaya katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, sasa umoja huo wenye nchi wanachama 27 unasita kukaribisha wanachama wapya. Labda alie na maoni tofauti ni waziri mkuu mpya wa Uingereza David Cameron.
"Ninapofikiria yale yaliyofanywa na Uturuki kama mshirika wa NATO kuilinda Ulaya na mchango wake wa hivi sasa nchini Afghanistan, hunikasirisha kuona jinsi uanachama wako unavyokumbana na vizingiti."
Cameron alitamka hayo mapema wiki hii mjini Ankara Uturuki na aliahidi kupigania uanachama wa Uturuki katika Umoja wa Ulaya. Kwa kweli hapo kinachozingatiwa na Uingereza sio Uturuki bali kuudhofisha Umoja wa Ulaya kama taasisi ya kisiasa. Uanachama wa Uturuki katika Umoja wa Ulaya ni mada mojawapo itakayojadiliwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Guido Westerwelle alie ziarani nchini Uturuki.
Mwandishi:Brand,Katrin/ZPR
Mhariri: Mtullya Abdu.