1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mvutano wa ubingwa wa AFCON kati ya Senegal na Morocco

Saleh Mwanamilongo
19 Machi 2026

Bodi ya rufaa ya Shirikisho la Soka la Afrika, CAF yainyang'anya Senegal ubingwa wa Michuano ya Mataifa ya Afrika, AFCON na kuitangaza Morocco kuwa mabingwa.

Kombe la Afrika 2025 | Fainali | Senegal dhidi ya Morocco | Sadio Mané anasherehekea na kombe
Senegal yanyang'anywa ubingwa wa AFCONPicha: Sebastien Bozon/AFP/Getty Images

Bodi ya rufaa ya CAF imeiondolea Sénégal ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika AFCON, miezi miwili baada ya kushinda fainali mjini Rabat. Katika taarifa iliyotolewa usiku wa kuamkia leo, CAF ilieleza kuwa imechukua uamuzi wa kuitangaza Senegal kuwa imepoteza kwa kufungwa, hivyo matokeo ya mechi yakarekebishwa kuwa ushindi wa Morocco wa mabao 3-0.

Shirikisho la soka la Senegal limepinga vikali uamuzi huo, likiuita kuwa si wa haki, wa kiholela na unaotia doa soka la Afrika. Limeongeza kuwa litakata rufaa haraka iwezekanavyo katika bodi ya usuluhishi ya Shirikisho la Soka Duniani FIFA. Abdoulaye Seydou Sow, katibu mkuu wa Shirikisho la Soka la Senegal, amesema kuwa nchi yake haitarudi nyuma na kwamba sheria iko upande wao.

Uamuzi huu pia umeibua hisia kali kwenye mitandao ya kijamii. Mchezaji wa Senegal Moussa Niakhaté alichapisha picha akiwa ameshika kombe hilo, akisema kwa hasira: "Njoo mlichukue! Wamechanganyikiwa!" : Kauli iliyoungwa mkono na wachezaji wengine wa timu hiyo.

“Kanuni za mchezo zinasema uamuzi wa Refa ni wa mwisho”

Senegal yavuliwa ubingwa AFCON, Morocco yatangazwa mshindiPicha: Mosa'ab Elshamy/AP Photo/dpa/picture alliance

Ikumbukwe kuwa fainali hiyo iliyochezwa Rabat tarehe 18 Januari iligubikwa na vurugu. Wachezaji wa Senegal walitoka uwanjani kupinga maamuzi ya refa, baada ya bao lao kukataliwa na penalti kutolewa kwa Morocco.

Baada ya dakika kadhaa za sintofahamu, mchezo uliendelea na Senegal ilishinda bao 1-0 kupitia Pape Gueye.

Hata hivyo, CAF imetumia kanuni zake zinazosema kuwa timu inayotoka uwanjani kabla ya mwisho wa mechi, inaweza kuhesabiwa kuwa imepoteza.

Kwa upande wake, Shirikisho la Soka la Morocco limesema halikupinga ushindi wa uwanjani bali lilitaka tu sheria zifuatwe.

Suala hili linafanana na tukio la mwaka 2019 ambapo Espérance Sportive de Tunis ilitangazwa bingwa baada ya wapinzani wao Wydad Casablanca kuondoka uwanjani wakipinga hitilafu ya mfumo wa kuhakiki wa VAR.

“Hakuna mtu ambaye angeweza kufikiria taarifa kama hiyo miezi miwili baada ya fainali,” alisema kocha mkongwe Claude Le Roy, aliyewahi kuiongoza Timu ya taifa ya Senegal kati ya mwaka 1988 na 1992.

“Kwa miaka mingi, maamuzi yote ya Refa yamepuuzwa na CAF,” alisema kupitia televisheni ya Ufaransa.

Wakati huo huo, kesi ya rufaa ya mashabiki 18 wa Senegal waliokamatwa kufuatia vurugu za fainali hiyo imeahirishwa hadi tarehe 30 Machi. Bila shaka, mgogoro huu utaendelea kuzua maswali kuhusu haki, kanuni na mustakabali wa soka barani Afrika.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW