1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaYemen

Mvutano mpya Yemen watishia Ghuba ya Arabuni

12 Desemba 2025

Kuongezeka kwa hali ya mvutano nchini Yemen kunatishia kuzuka upya vita vya wenyewe kwa wenyewe na kusababisha mgogoro mkubwa katika eneo zima la Ghuba ya Arabuni.

Yemen Aden 2025 |
Waasi wanaotaka kujitenga wanasema watakuwa nguzo ya juhudi zozote zinazounga mkono usalama na uthabiti nchini Yemen.Picha: Fawaz Salman/REUTERS

Kundi la wanamgambo wanaotaka kujitenga linaloungwa mkono na Umoja wa Falme za Kiarabu, limechukua udhibiti wa sehemu kubwa ya majimbo ya Hadhramaut na Mahra, vikiwemo vituo vya mafuta na bandari muhimu. Hatua hii imevunja utulivu wa muda uliokuwepo tangu 2022, baada ya pande zinazopigana kufikia makubaliano ya kusitisha vita nchini Yemen.

Msimamo wa Saudi Arabia

Rashad al-Alimi, mwenyekiti wa Baraza la Uongozi, serikali inayotambuliwa kimataifa ya Yemen, amewataka waasi hao wanaotaka kujitenga kukabidhi madaraka kwa mamlaka za mitaa na kuonya juu ya umwagaji damu zaidi. Aidha al-Alimi amesisitiza kuwa kipaumbele kinapaswa kuwa mapambano dhidi ya Wahouthi, ambao wamekuwa wakiidhibiti kaskazini mwa Yemen kwa zaidi ya muongo mmoja.

Saudi Arabia, ambayo iliongoza vita dhidi ya Wahouthi kwa miaka kadhaa kabla ya kufikia makubaliano na kundi hilo linaloungwa mkono na Iran, imetuma ujumbe Hadhramout kukutana na gavana na viongozi wa kikabila ili kupunguza mvutano. Hata hivyo, wachambuzi wanasema Saudi Arabia "haijaridhishwa kabisa” na hatua ya waasi hao, huku Umoja wa Falme za Kiarabu ukionekana kutanuwa ushawishi wake katika mzozo wa Yemen.

Al-Alimi alionya kuwa hatua za upande mmoja za waasi wanaotaka kujitenga zinaweza kuathiri vibaya uchumi dhaifu wa Yemen, akibainisha kuwa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) limesitisha shughuli zake za kuimarisha uchumi kufuatia mvutano huo.

Tamko la waasi wanaotaka kujitenga

Wakati huohuo, waasi hao na washirika wao wametoa tamko wakisisitiza kutokubali kurudi nyuma na badala yake kuyataka mataifa ya ukanda huo na jumuiya ya kimataifa kutambuwa haki ya Waye­meni wa kusini kuwa na taifa lao huru.

Kiongozi wa Ofisi ya Kisiasa ya Baraza la Mpito la Kusini, Anis al-Sharafi amesema

Wapiganaji wanaohusishwa na Baraza la Mpito la Kusini la Yemen wakishika doria.Picha: SALEH OBAIDI/AFP

"Huenda tunatoa kipaumbele kwa malengo yetu kusini, lakini hatutahatarisha usalama wa  mataifa ya Kiarabu, wala hatutahatarisha usalama na uthabiti wa Saudi Arabia."

"Tutakuwa nguzo ya juhudi zozote zinazounga mkono usalama na uthabiti wa Ufalme wa Saudi Arabia, na ndugu zetu katika Ufalme wa Oman na nchi za Ghuba kwa ujumla, pamoja na usalama wa Bahari ya Shamu na usalama wa bahari. Tutakuwa na msaada wa mkubwa kwao."

Kwa sasa waasi wanaotaka kujitenga na makundi yanayoungwa mkono na Umoja wa Falme za Kiarabu wanadhibiti sehemu kubwa ya kusini mwa Yemen, ikiwemo miji ya bandari na visiwa muhimu.

Hali hii inavuruga makubaliano ya kisiasa miongoni mwa washirika wanawaopinga Wahouthi na kuiweka Yemen katika hatari ya kuingia tena kwenye vita vikubwa vya wenyewe kwa wenyewe, ambavyo vinaweza kuathiri utulivu wa Ghuba nzima ya Arabuni na masoko ya kimataifa ya mafuta.

//AFP, AP

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW