Mvutano wa kisiasa waongezeka nchini Kongo
20 Mei 2026
Hayo yanajiri wakati Rais Felix Tshisekedi na chama tawala cha Union for Democracy and Social Progress wakisema Katiba ya sasa inahitaji maboresho, upinzani na mashirika ya kiraia wanaonya kuwa hatua hiyo inaweza kufungua njia ya kuondoa ukomo wa mihula. Katika hatua mpya ya kupinga mpango huo, viongozi wa upinzani wameunda muungano mpya uitwao "C64” wenye lengo la kuratibu kampeni dhidi ya kile wanachokiita jaribio la kubadili Katiba kwa maslahi ya kisiasa.
Katika ukumbi uliokuwa umejaa tahadhari na hali ya wasiwasi mjini Kinshasa, viongozi wa vyama vya upinzani pamoja na mashirika ya kiraia walikusanyika kujadili mustakabali wa Katiba ya nchi hiyo. Kwao, lengo kuu ni kulinda sheria mama dhidi ya kile wanachodai kuwa ni jaribio la kugeuza mfumo wa kidemokrasia wa nchi.
Miongoni mwa waliozungumza ni wakili Nicolas Lenga, kada wa chama cha Envol, ambaye alisema hatua za serikali zinaonyesha mwelekeo wa kimabavu unaotishia misingi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
"Tukiamini kwamba mwelekeo wa kimabavu ulioanzishwa na utawala wa Bwana Félix Tshisekedi kupitia mpango wake wa kubadilisha Katiba ni kitendo cha uasi dhidi ya Jamhuri na tangazo la vita kwa wananchi wa Kongo… ni wajibu wa kila Mkongo kusimama ili kulinda Katiba na mamlaka ya taifa.”
Mvutano huu unaweza kuongeza mgawanyiko mkubwa zaidi Kongo
Kwa upinzani, msingi wa mapambano hayo unatokana na kifungu cha 64 cha Katiba ya DR Congo, kinachowapa wananchi wajibu wa kumpinga mtu yeyote anayechukua au kutumia madaraka kinyume cha Katiba. Viongozi wa muungano wa C64 wanasema wanataka kuhamasisha wananchi kulinda misingi ya demokrasia kabla hali haijazidi kuwa mbaya.
Nicolas Lenga anasema hatua hiyo siyo harakati ya kisiasa pekee, bali ni wito wa kizalendo kwa Wakongo wote ndani na nje ya nchi.
"Tunatoa wito rasmi kwa kila Mkongomani, popote alipo, kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa kifungu cha 64 cha Katiba yetu kinachosema: Kila Mkongomani ana wajibu wa kumpinga mtu yeyote au kikundi chochote cha watu wanaochukua mamlaka kwa nguvu au kuvitumia kinyume na masharti ya Katiba hii.”
Hata hivyo, wachambuzi wa siasa wanaonya kuwa mvutano huu unaweza kuongeza mgawanyiko mkubwa zaidi nchini humo. Wanasema mjadala wa Katiba tayari umeanza kuamsha hofu kuhusu utulivu wa kisiasa kuelekea mwisho wa muhula wa sasa wa Rais Tshisekedi.
Mchambuzi wa siasa za Afrika ya Kati, Josephat Musamba, anaamini kuwa hatua ya kubadilisha Katiba inaweza kuibua kipindi kigumu cha kutotabirika kisiasa iwapo hakutakuwa na mazungumzo ya kitaifa na maridhiano.
Kwa sasa, mjadala huo unaendelea kugawa maoni nchini DR Congo. Wafuasi wa serikali wanaamini mabadiliko ya Katiba yanaweza kusaidia kuimarisha taasisi za taifa na kuchochea maendeleo, huku upinzani ukisisitiza kuwa hatua hiyo ni tishio kwa demokrasia na utawala wa sheria.
Huku mvutano wa kisiasa ukiendelea kuongezeka, wananchi wa Kongo wanaendelea kujiuliza mustakabali wa demokrasia yao na iwapo taifa hilo litaweza kuepuka mgogoro mwingine wa kisiasa kabla ya uchaguzi mkuu ujao.