1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Janga

Mvutano wa kiusalama Ghuba ya Uajemi waathiri usafirishaji

27 Aprili 2026

Mvutano wa kiusalama katika Ghuba ya Uajemi unaendelea kuathiri kwa kiasi kikubwa usafirishaji wa kimataifa, huku maelfu ya mabaharia wakikwama baharini kutokana na mashambulizi ya kijeshi na vikwazo vya usafiri.

Symbolbild | Philippinen |  Covid-19 | Schiffsbesetzungen kommen nicht weg
Licha ya kuwepo kwa makubaliano dhaifu ya kusitisha mapigano kati ya Marekani na Iran, hali bado ni ya tahadhari kubwa. Picha: Aaron Favila/AP Photo/picture-alliance

Mlango huo wa Bahari ni njia muhimu ya kupitisha karibu  asilimia 20 ya mafuta na gesi duniani.

Kwa takribani wiki nane sasa, nahodha wa meli kutoka India, Rahul Dhar, pamoja na wafanyakazi wake wamekwama katika eneo hilo, wakishuhudia milipuko ya mara kwa mara ya droni na makombora. Dhar anasema ingawa morali ya wafanyakazi bado ipo juu, dalili za msongo zinaanza kuonekana wanapoendelea na shughuli zao za kila siku ndani ya meli.

"Tangu wakati mzozo huu ulipoanza tarehe 28 Februari, kuna zaidi ya mabaharia wa India 22,000 hadi 23,000 waliokwama ndani ya eneo la mapigano. Ofisi yetu inaratibu mawasiliano na waliokwama katika bandari mbalimbali za Iran kama Bandar Abbas, Sirri, Lavan na Khorramshahr."

Dhar anaongeza kuwa licha ya kuwepo kwa makubaliano dhaifu ya kusitisha mapigano kati ya Marekani na Iran, hali bado ni ya tahadhari kubwa. Wafanyakazi wamekuwa wakishuhudia makombora na droni zikizuiliwa angani karibu nao, hali inayoongeza hofu. Hata hivyo, mawasiliano ya mtandao yamewasaidia kuwasiliana na familia zao na kuwapa faraja.

Idadi ya meli zinazopita Hormuz imepungua kwa kiasi kikubwa

Kwa mujibu wa takwimu za usafirishaji baharini, idadi ya meli zinazopita katika njia hiyo imepungua kwa kiasi kikubwa - kutoka zaidi ya meli 130 kwa siku kabla ya mzozo hadi takribani meli 80 kwa wiki katikati ya Aprili. Tangu kuanza kwa mapigano, makumi ya meli zimeshambuliwa, na  Umoja wa Mataifa  umeripoti kuwa takribani mabaharia 10 wameuawa.

Licha ya Rais wa Marekani Donald Trump kuongeza muda wa kusitisha mapigano, Marekani imeendelea kuzuia bandari za Iran, ambayo nayo imejibu kwa kukaza udhibiti wake, ikiripotiwa kushambulia meli na kuzikamata nyingine.

Reza Muhammad Saleh, afisa mkuu kutoka Indonesia aliyekwama karibu na Oman kwenye meli inayopeperusha bendera ya Ugiriki, amesema walishuhudia mlipuko wa droni karibu na bandari muda mfupi baada ya kuwasili mwezi Machi. Matukio hayo yaliwalazimisha wafanyakazi kukimbilia mafichoni mara kadhaa.

"Ilikuwa hali ya wasiwasi mkubwa sana; hadi sasa bado tuna hofu kuwa mapigano yanaweza kuanza tena na kutokea shambulizi lingine la ndege isiyo na rubani, lakini kwa sasa bado ni salama."

Meli hiyo yenye wafanyakazi 24 kutoka Indonesia, India, nchi za Kiarabu na Ethiopia kwa kawaida hupitia njia hiyo mara moja au mbili kwa mwezi, lakini sasa  inahitaji kibali maalum kutoka Iran, huku kampuni nyingi zikikataa kuhatarisha safari bila uhakika wa usalama.

Mashirika ya kimataifa, ikiwemo Shirika la Usafirishaji Baharini la Umoja wa Mataifa, yametoa wito wa kuanzishwa kwa njia salama ya kupitisha meli katika eneo hilo. Hata hivyo, hatari ya mashambulizi na uwepo wa mabomu ya baharini vinaendelea kufanya safari hiyo kuwa hatari kubwa.

 

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW