Mvutano waibuka kati ya Umoja wa Ulaya na Poland
19 Oktoba 2021Rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesema uamuzi wa mahakama ya Poland ni tishio kwa misingi ya Umoja huo na kwamba hawatakaa kimya.
Msuguano kati ya Poland na Umoja wa Ulaya unaendelea kufukuta kufuatia uamuzi wa mahakama ya katiba ya Poland kupinga ukuu wa sheria za Umoja wa Ulaya juu ya sheria za nchi hiyo, ikisema baadhi ya sheria za Umoja huo zinakinzana na katiba ya Poland.
Akiwahutubia wabunge wa Umoja wa Ulaya mjini Strasbourg, Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja huo, Ursula von der Leyen, amesema ana wasiwasi mkubwa juu ya uamuzi huo wa mahakama ya katiba ya Poland, akisema uamuzi huo ni changamoto ya moja kwa moja kwa Umoja wa EU na kwamba uamuzi huo unadhoofisha ulinzi wa uhuru wa mahakama.
Soma pia: Poland yakosolewa kuwarejesha wakimbizi kinyume cha sheria
Von der Leyen amesema, "Utawala wa kisheria ndio unaofungamanisha umoja wetu."
Uhusiano kati ya Poland na Umoja wa Ulaya umetetereka katika siku za hivi karibuni baada ya majaji wa Poland kuamua kuwa sheria za nchi hiyo zinafaa kupewa kipaumbele zaidi juu ya sheria za Umoja wa Ulaya. Uamuzi huo wa mapema mwezi huu ulichochea mvutano juu ya viwango vya demokrasia kati ya serikali ya mrengo wa kulia ya Poland na Brussels.
EU yasema uamuzi wa mahakama ya Poland ni kitisho kwa utawala wa sheria
Mvutano huo ulidhihirika hadharani leo Jumanne katika bunge la Umoja wa Ulaya baada ya Waziri Mkuu wa Poland Mateusz Morawiecki kutetea msimamo wa nchi hiyo kwamba sheria za nchi yake.
"Haikubaliki kuweka uamuzi kwa mtu mwengine bila msingi wa kisheria. Haikubaliki kutisha mtu kwa kutumia kigezo wa fedha, kuzungumza juu ya vikwazo ama kutumia lugha mbaya dhidi ya baadhi ya nchi. Napinga lugha hii ya vitisho au kulazimishwa. Napinga wanasiasa kuitisha Poland"
Hata hivyo Morawiecki amesisitiza kuwa Poland inaheshimu mikataba yote ya Umoja wa Ulaya na kupuzilia mbali kauli za wapinzani wa serikali yake ambao wanahofia kuwa huenda uamuzi wa mahakama ya Poland ukafungua uwezekano wa nchi hiyo kujiondoa kutoka Umoja wa Ulaya, Polexit.
Soma pia: Rais wa Poland ana corona, awaomba radhi aliokaribiana nao
Waziri Mkuu huyo wa Poland amesema, "Hatupaswi kueneza uwongo juu ya Poland kuondoka kutoka Umoja wa Ulaya", na kuongeza kuwa nchi yake haitayumbusishwa na vitisho na kuwa anatarajia mazungumzo yenye tija.
Kiini cha mvutano kati ya Poland na EU ni juu ya nani anayepaswa kuwa na nguvu kubwa zaidi ndani ya Umoja huo, je, ni nchi juu ya raia wake ama taasisi za Umoja wa Ulaya juu ya nchi wanachama? Suala hilo ndio kichocheo kikuu cha Uingereza kujiondoa kutoka Umoja wa Ulaya na pia limesababisha minong'ono katika baadhi ya mataifa ya mashariki na Ulaya ya kati kama vile Poland na Hungary.