1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mvutano wazidi makali kati ya Ufaransa na Italia

Oumilkheir Hamidou
8 Februari 2019

Ufaransa imemwita balozi wake nchini Italia kufuatia taarifa kadhaa za "kuchukiza" zilizotolewa na viongozi wa Italia. Huu ni mzozo wa aina pekee kuwahi kutokea kati ya nchi mbili wanachama wa Umoja wa Ulaya,

Italiens Liga veranstaltet eine Kundgebung in Rom - Matteo Salvini
Picha: Reuters/A. Bianchi

Viongozi wawili wa serikali ya Italia, waziri wa mambo ya ndani Matteo Salvini na makamo waziri mkuu Luigi Di Maio, washika bendera wa serikali ya siasa kali za kizalendo nchini Italia hawakukawia kusema wako tayari kukutana na rais Emmanuel Macron na serikali ya Ufaransa.

"Kwa muda sasa nimesema niko tayari kwenda kwa mguu Paris, kwasababu kuna kadhia tatu za masilahi ya Italia zinazobidi kupatiwa ufumbuzi," amesema waziri wa mambo ya ndani Matteo Salvini na kuongeza. "NImemualika waziri mwenzangu wa Ufaransa tukutane wiki inayokuja Pescara kulifumbua tatizo lililoko."

Wanaharakati wa vuguvugu la vizibao vya manjanoPicha: Getty Images/AFP/Z. Abdelkafi

Italia yanyunyizia mafuta katika cheche za moto

Lakini kwa viongozi wa serikali ya Ufaransa, matamshi ya uchokozi ya viongozi wa Italia yamekithiri. Duru za kidiplomasia zinasema, uamuzi wa kumrejesha nyumbani balozi kwa ajili ya "mashauriano" ni tukio la aina pekee kuwahi kushuhudiwa kati ya Ufaransa na jirani yake Italia tangu mwaka 1945, sawa na matamshi makali ya mwanachama wa Umoja wa Ulaya dhidi ya mwenzake.

Viongozi hao wawili wa Italia wamezidisha maudhi na matusi dhidi ya viongozi wa Ufaransa na kufika hadi ya kuwasifu wanaharakati wa vuguvugu la vizibao vya manjano wanaomtaka rais Macron ajiuzulu. "Akiondoka tu, mambo yatakuwa mazuri" alisema Salvini mwezi uliopita na kumtuhumu rais Macron kuiongoza nchi dhidi ya wananchi.

Mazungumzo ya Jumanne iliyopita kati ya naibu waziri mkuu wa Italia Luigi Di Maio, na wanaharakati wa vizibao vya manjano ndio yaliyonyunyizia mafuta katika cheche za moto.

Waziri wa mambo ya ndani wa italia Matteo Salvini na waziri mwenzake wa Poland Joachim BrudzinskiPicha: picture-alliance/NurPhoto/M. Wlodarczyk

 Salvini atuhumiwa  kutaka kuligawa bara la Ulaya

"Kuwa na misimamo tofauti katika suala fulani ni kitu kimoja, kuutumia uhusiano kwa malengo ya uchaguzi ni kitu chengine amesema msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje wa Ufaransa.

Matteo Salvini anatuhumiwa kubuni kambi ya siasa kali za mrengo wa kulia barani Ulaya, dhidi ya wenye kupigania Umoja wa Ulaya wanaaoongozwa na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, kuelekea uchaguzi wa Ulaya utakaoitishwa Mei 26, 2019.

 

Mwandishi: Hamidou Oumilkheir/AP/AFP

Mhariri: Yusuf Saumu

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW