1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwaandishi Samson Kasumba aachiwa kwa dhamana

22 Aprili 2020

Polisi imemwachia kwa dhamana mwanahabari wa Uganda Samson Kasumba baada ya kumfahamisha kuwa anafanyiwa uchunguzi kuhusu kesi ya uchochezi. Hata hivyo wakili wa mwanahabari huyo anasisitiza kuwa mashtaka hayo ni batili

Uganda | Samson Kasumba | Journalist
Picha: DW/L. Emmanuel

Siku ya Jumanne mchana kutwa, mwandishi habari nchini Uganda pamoja na mawakili wa Samson Kasumba walifuatilia jinsi polisi ilivyokuwa ikishughulikia kukamatwa kwa mwanahabari Samson Kasumba.

Hatimaye usiku, mwandishi huyo aliachiwa kwa dhamana ya polisi bila kufahamishwa hasa makosa aliyoyatenda ila tu kuambiwa ni makosa ya uchochezi ambayo yeye na wengine wanadaiwa kuhusika.

Wakili na mtetezi maarufu wa haki za binadamu Nicholas Opiyo ndiye aliyeongoza mawakili wengine kuhakikisha kuwa mteja wao halali korokoroni siku ya pili. Wakili huyo amesisitiza kuwa yamkini polisi hawana ushahidi wa kutosha kuhusiana na kesi hiyo na hatashangaa kama atafunguliwa mashtaka mengine tofauti.

"Si muhimu na wala sio suali linalohitaji kushughulikiwa hasaa katika mazingira ambapo hatuelezwi wazi wazi kuhusu makosa yake. Kwahivyo hakuna haja ya kusmhikilia Samson kwa muda mrefu," alisema Nicholas Opiyo.

Mazingira ya kukamatwa kwa mwanahabari huyo siku ya Jumatatu jioni yamewatia wanahabari katika mashaka makubwa wakishangaa ni nini hasa kilichomsababisha kukamatwa.

Samson asema hakupigwa wala kunyanyaswa na polisi alipokuwa ndani

Picha: Getty Images/AFP/I. Kasamani

Katika kikao cha wanahabari, naibu msemaji wa polisi ametakiwa kuelezea zaidi kuhusu mashtaka dhidi ya mwanahabari mwenzao ili nao wasije wakatumbukia katika mtego huo katika kipindi hiki ambapo taifa linapambana dhidi ya ugonjwa wa COVID-19.

"Tukizungumzia Propaganda hatari hatuwezi kutoa ufafanuzi zaidi kuhusu uchunguzi wetu na mahakama haingependa tufanye hivyo," alisema Polly Namaye 

Baada ya kupewa dhamana, Samson alisindikizwa hadi nyumbani kwake na polisi na hapo ndipo alipopata uhuru kamili wa kuelezea kuhusu masaibu yake katika kipindi alipokamatwa.

"Jambo muhimu katika suala hili ni kufahamu kuwa unapofanya kazi yatu ya uanahabari kuna watu unawakasirisha lakini polisi wamekuwa wema na sikunyanyaswa wala kupigwa," alisema Samson.

Awali siku ya Jumanne, polisi walikwenda na Kasumba nyumbani kwake na kuipekua. Baadaye waliondoka na kompyuta yake pamoja na stakabadhi kadhaa huku watoto wa kike walimlilia baba yao. Kasumba ametakiwa kwenda kwa kituo cha polisi kila siku huku uchunguzi wa mashtaka dhidi yake na wengine asiowajua ukiendelea.

Chanzo: Lubega Emmanuel DW Kampala.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW