Mwafaka kutiwa saini Zimbabwe
15 Septemba 2008Mugabe na Tsvangirai wiki iliopita walifikia makubaliano ya kukomesha mzozo mzito wa kisiasa uliochochewa na uchaguzi tata wa rais na kuchaguliwa tena bila ya kupingwa kwa kiongozi mkongwe wa nchi hiyo katika marudio ya uchaguzi ya mwezi wa Juni.
Wananchi wa Zimbabwe wanataraji makubaliano hayo yatakuwa hatua ya kwanza ya kusaidia kulinusuru taifa hilo lililokuwa limestawi huko nyuma kutoka kusambaratika kiuchumi,kupanda kwa gharama za maisha kufikia zaidi ya asilimia milioni 11 na mamilioni ya Wazimbabwe kukimbilia nchi jirani za kusini mwa Afrika.
Chini ya makubaliano hayo yaliosimamiwa na Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini Tsvangiari atakuwa waziri mkuu na mwenyekiti wa kusimamia shughuli za baraza la mawaziri wakati Mugabe ataendelea kushikilia wadhifa wa Urais.
Chama cha MDC imeelezwa kuwa kinataka kudhibiti wizara za mambo ya ndani ili kusimamia shughuli za polis,serikali za mitaa,mojawapo ya wizara za sheria,habari na wizara ya fedha ili kuweza kuwa na jukumu la kuokowa uchumi.