1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Arusha: Waathirika wasubiri fidia au hata faraja kutoka mamlaka

Veronica Natalis
27 Oktoba 2026

Mwaka mmoja baada ya machafuko ya uchaguzi wa Tanzania, familia za waliopoteza maisha jijini Arusha zinaendelea kuomboleza. Baadhi zinasema hazijapata fidia wala kufarijiwa na mamlaka za serikali.

Tanzania Arusha 2025 | Maandamano baada ya uchaguzi wa wabunge kutokana na madai ya kasoro za uchaguzi
Arusha ilikuwa miongoni mwa maeneo ya Tanzania yaliyoshuhudia maandamano na vurugu wakati wa uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.Picha: AP Photo/picture alliance

Kila anapomkumbuka mwanawe mwenye umri wa miaka 19, Living Mtena hukumbuka pia siku ambayo maisha ya familia yake yalibadilika. Kijana huyo alipigwa risasi akiwa pamoja na baba yake kazini jijini Arusha, wakati wa machafuko yaliyotokea siku ya uchaguzi mkuu wa Tanzania, Oktoba 29, 2025.

Mtena anasema mwanawe alifariki dunia siku mbili baadaye, baada ya kupelekwa katika Hospitali ya Mount Meru kwa matibabu.

"Tulikuwa pamoja kazini. Alipoingia ndani kuchukua nyundo, alipigwa risasi nje ya ofisi yangu,” anasimulia Mtena.

Anasema baada ya mwanawe kupigwa risasi, alimchukua na kwenda naye kwa babu yake. Hata hivyo, waliambiwa kuwa serikali ilikuwa imeelekeza majeruhi wote wapelekwe Hospitali ya Mount Meru.

"Tulipewa ambulensi na kupelekwa huko, lakini kwa bahati mbaya tarehe 31 alifariki dunia,” anasema.

Katika baadhi ya maeneo ya Arusha, watu walijeruhiwa na wengine kupoteza maisha wakati wa machafuko ya uchaguzi.Picha: AP Photo/picture alliance

Maisha yaliyobadilika baada ya msiba

Mwaka mmoja baada ya matukio hayo, Mtena anasema bado anaishi na maumivu ya kumpoteza mwanawe. Msiba huo, anaeleza, umeathiri afya yake na kumwongezea majukumu ya kifamilia.

"Kwa namna moja au nyingine, maisha yangu yalibadilika kabisa. Nimepata maradhi ambayo sikuwa nayo awali, ikiwemo shinikizo la damu,” anasema.

Mwanawe alikuwa kwenye mahusiano na binti ambaye wakati huo alikuwa na ujauzito wa miezi miwili. Mtena anasema sasa anamsaidia binti huyo pamoja na kumlea mjukuu wake mwenye umri wa miezi mitano.

Kwa mujibu wake, mwenyekiti wa mtaa ndiye kiongozi pekee wa serikali aliyemfariji na kumpa mkono wa pole baada ya msiba huo.

"Sina cha kupoteza, kwa sababu tayari nilishapoteza,” anasema Mtena.

Mwaka mmoja baada ya matukio hayo, baadhi ya familia za wahanga jijini Arusha bado zinaomboleza na kutafuta majibu kuhusu vifo vya wapendwa wao.Picha: AP Photo/picture alliance

Familia nyingine bado inatafuta majibu

Katika makaburi ya Njiro jijini Arusha amezikwa David Baltazari, kijana mwingine aliyefariki baada ya kupigwa risasi wakati wa matukio ya Oktoba 29, 2025. Alikuwa na umri wa miaka 23.

Kaka yake, Baraka Baltazari, anasema familia yao haijawahi kupata fidia wala kutembelewa na mwakilishi yeyote wa serikali ili kuifariji.

"Hakujakuwa na fidia yoyote wala kutembelewa na mtu yeyote kutoka serikalini. Kilichotokea hakikuwa jambo zuri. Alikuwa bado kijana mdogo anayejitafuta maishani,” anasema Baraka.

Anaongeza kuwa familia ilipitia wakati mgumu hata kuupata mwili wa ndugu yao. "Kulikuwa na matukio mengi ya huzuni, na hata kuupata mwili wake ilikuwa kazi ngumu sana.”

Mamia walipoteza maisha

Siku ya uchaguzi, mamia ya waandamanaji walishuhudiwa katika eneo la Sanawari, kando ya barabara kuu inayounganisha Arusha na Moshi. Maandamano pia yaliripotiwa katika maeneo mengine ya jiji la Arusha na baadhi ya mikoa nchini Tanzania.

Waandamanaji waliingia mitaani kupinga kufanyika kwa uchaguzi kabla ya kufanyika mageuzi. Wakati vyombo vya dola vilipowakabili waandamanaji, kuliripotiwa watu kupigwa risasi, wengine kujeruhiwa na mali kuharibiwa.

Ibada ya funga na ustahamilivu wa kidini

03:52

This browser does not support the video element.

Tume iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuchunguza matukio hayo iliripoti kuwa zaidi ya watu 500 walipoteza maisha. Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa zilizopo katika ripoti hii, mwaka mmoja baadaye hakuna watu waliotajwa rasmi kuwa wahusika wa matukio hayo wala kuwajibishwa kisheria.

Imehaririwa na:Iddi Ssessanga
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW