1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwaka mmoja Tanzania bila Magufuli

17 Machi 2022

Leo ni mwaka mmoja tangu rais wa Tanzania wa awamu ya tano, hayati John Magufuli alipofariki. Shughuli za hafla ya kumbukumbu hiyo zinaongozwa na Rais Samia Suluhu aliyeambatana karibu na viongozi wote wa serikali.

Tansania Amtseid des Präsidenten John Pombe Magufuli
Picha: Tanzania Presidential Press Service

Leo Watanzania wanaadhimisha mwaka mmoja tangu Rais wa awamu ya tano dokta John Pombe Magufuli alipoaga dunia, katika kumuenzi Rais huyo ambaye mara zote alijipambanua kama mtetezi wa wanyonge, shughuli mbalimbali zimefanyika ikiwemo ibada maalumu iliyofanywa kijijini kwake huko Chato na  kutolewa nasaha kutoka kwa viongozi mbalimbali waliohudhuria kumbukumbu hiyo.

Akiongoza ibada hiyo iliyohudhuriwa na waumini wa Imani mbalimbalil, Askofu mkuu wa Jimbo la Geita, Flavian Kissala aliwahubiria waumini kuhusu maisha ya binadamu hapa duniani na hatma ya safari yao kuelekea kwa muumba wao.

Soma pia: Samia: "Naendeleza kazi ya mtangulizi wangu"

Alisema Rais Magufuli kama ilivyo kwa binadamu mwingine kuna mengi aliyoyapitia lakini alijaribu kutimiza wajibu wake kama kiongozi wa taifa, ingawa kuna uwezekano wa kuwepo mapungufu na hayo yanadhihirisha kuwa yeye alikuwa binadamu kama binadamu mwingine.

Rais Samia: Tutaendeleza alipoishia Rais Magufuli

Rais wa Tanzania Samia Suluhu HassanPicha: Eric Boniphase/DW

Wengi waliozungumza kwenye kumbukumbu hii, walimtaja hayati Magufuli kama kiongozi hodari na mchapa kazi aliyebeba dira ya taifa.

Rais samia Suluhu Hasan ambaye alichukua hatamu baada ya kifo hicho kwa mujibu wa katiba ya taifa hilo ambae ameongoza watanzania katika kumbukumbu hiyo alisema, kwake binafsi kuondokewa na Magufuli ilikuwa ni mshtuko mkubwa huku akiwaza namna gani ataendeleza maono ya mtangulizi wake.

Alisema "ilikuwa ni dhamana kubwa inayotishwa mabegani,nilijiuliza nitaanzia wapi?" Katika kumbukumbu hiyo amewaahidi Watanzania kuendeleza miradi yote ambayo ilianzwa na serikali ya awamu ya tano wakati huo akiwa makamu wa Rais.

Soma pia: Utendaji wa Magufuli wazua mjadala mzito Tanzania

Aidha Rais Samia ameongeza kuwa hakuna maendeleo yoyote ambayo yalianzishwa na mwendazake ambayo yatasimama katika mkoa wa Geita ikiwemo wilaya ya Chato ambapo ndipo Rais Magufuli alikulia na kuianza safari yake ya kisiasa, kadhalika kuzikwa huko.

"Vilevile kiwanja cha ndege cha Chato kimeendelea kukamilika kwa zaidi ya asilimia 90"

Wachambuzi: Rais Magufuli alijijenga kwa wananchi wa kawaida lakini akaporomosha diplomasia

Raia wa Tanzania wakitoa heshima zao za mwisho kwa hayati John MagufuliPicha: Mwanza Dotto Bulendu/DW

Miaka takriban sita ya Rais Magufuli mamlaka ilitafsiriwa kama shubiri katika baadhi ya nyanja ikiwemo haki haki ya kisiasa ilitajwa kuzorota kwa kiwango kikubwa na hata kuzua hofu miongoni mwa vyama vya upinzani katika kutekeleza majukumu yao kama vyama vya siasa.

Kupigwa marufuku kwa mikutano ya hadhara iliweza kurudisha nyuma shughuli za kisiasa, hatua iliotafsiriwa kuwa ni kufifisha mfumo wa democrasia ambao nchi imejichagulia katika kupata viongozi wake.

Goodluck Ng'ingo mchambuzi wa masuala ya siasa, uchumi na diplomasia anasema,hofu ilizuka miongoni mwa wanansiasa,ukosoaji wa mamalaka ulitoweka wengi wakiohifia juu ya hatima yao, hatua iliozorotesha utamaduni wa kukosoana na kurekebishana kama taifa na badala yake ikabaki mfumo wa kusifia hata pale kulipokuwa na makosa.

"kwa sasa tunaona vyama vya siasa vinashirikishwa,tofauti na hapo mwanzo vilijiweka mbali kabisa" Alisema Goodluck katika mazungumzo na DW ikiwa ni mwaka mmoja tangu kifo cha Rais John Magufuli.

Kwa upande mwingine wanaharakati wa haki za binadamu kupitia asasi za kiraia zilitafsiri miaka hiyo sita kama ni msimu mbaya kwao kutokana na kubadilishwa kwa sheria na kuwekwa  sheria ambazo ziliwaminya katika utendaji kazi wao.

Soma pia: Hayati Magufuli aagwa nyumbani kwake Chato

Hatua hii wanaiona ni kama ililenga kuwapora nguvu yao na sauti yao iliowakikisha umma dhidi ya mamlaka waliokuwa nayo katika wamu zilizopita za uongozi.

Hellen Kijo Bisimba aliyekuwa mkurugenzi wa kituo cha sheria na haki za binadamu nchini Tanzania aliiambia Dw kuwa katika kipindi hiki cha mwaka mmoja hana zuri ambalo anaweza kujivunia juu ya Rais Magufuli. "Sitakuwa kwenye nafasi nzuri ya kumzungumzia katika mazuri ukiangalia eneo langu lilikuwa ni haki za binadamu sijaona maendeleo" Aliiambia DW:

Alipoulizwa kuhusu suala la miundombinu na kutetea wanyonge kama ilivyokuwa sera yake kadhalika nidhamu kwa watumishi wa umma Bisimba alisema kwa ufupi kwamba "Ilikuwa ni nidhamu ya woga ameondoka nayo."

Maoni mseto kutoka kwa wananchi

Kama alivyowahi kusema mwenyewe, angependa akukumbukwe kwa mema,  ndivyo baadhi ya wananchi wanavyoitazama siku hii wakikumbuka namna alivyoanzisha miradi mikubwa ya ujenzi wa madaraja, usafiri wa treni, ufufuaji wa shirika la ndege la taifa pamoja na ujenzi mkubwa wa bwawa la kufua umeme.

Baadhi ya wananchi wamesema bado pengo lake linaonekana katika maisha ya kila siku wakitolea mfano huduma za kijamii kuanza kuzorota, nidhamui ya watumishi wa umma si ya kuridhisha, huku huduma kama vile maji na umeme zimerudi katika mfumo ambao si  wa uhakika.

Wamemtaka Rais Samia kuhakikisha kwamba anakuwa mkali kwa baadhi ya watumishi ambao wanaleta uzembe pahala pa kazi na kunyanyasa wananchi.

Maadhimisho haya yanafanyika wakati Tanzania ikiwa imejipambanua kivinginge kutokana na sera mpya zinazochukuliwa na mrithi wake kuanzia kuanzisha mahusiano mapya na jumuiya ya kimataifa, uhuru wa vyombo vya habari na masuala ya kidemokrasia.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW