Mwaka wapili tangu kuwawa kwa Rafik Hariri-Lebanon
14 Februari 2007
Maalfu ya walebanon-wafuasi wa marehemu waziri mkuu Rafik Hariri, wamekusanyika wakati huu katika kitovu cha Beirut,kwenye kaburi la marehemu kwa ukumbusho wa mwaka wa pili tangu kuuliwa kwake.Mamia ya askari-jeshi wanashika zamu kuzuwia kuzuka fujo-siku moja baada ya mabomu 2 kuripuka na kuua watu 3 na kuwajeruhi wengine kadhaa.
Saad Hariri, mtoto wa mwanasiasa huyu wa madehebu ya sunni, alisema hapo kabla kuwa, mkusanyiko huu utaendelea licha ya mabomu yalioripuliwa jana na kuawa watu 3 na kuwajeruhi 20 wengine.
Saad Hariri na washirika wake wa vyama vya serikali ya muungano ya Lebanon wameitisha maandamano ya leo kuonesha mshikamano pia na serikali inayokabili changamoto kali kutoka upinzani unaoongozwa na Hizbollah kuiporomoa chini.
Serikali ya muungano ya Lebanon, ilinyoshea kidole Syria kwa miripuko ya mabomu ya jana ambayo pia inadaiwa ndio ilio nyuma ya kuuwawa Februari 14, mwaka juzi kwa waziri-mkuu mara 5 wa Lebanon, Rafik Hariri-tukeo ambalo liliongoza kuuliwa kwa viongozi kadhaa wasio marafiki wa Syria nchini Lebanon.
Syria imekuwa ikikanusha kuhusika kwa aina yoyote na mauaji ya Rafik Hariri, yaliochochea shinikizo ulimwenguni dhidi ya Syria ili iondoe majeshi yake kutoka Lebanon hapo 2005 baada ya kuwapo nchini kwa miaka 29.
Waziri mkuu wa Lebanon, Fouad Siniora ameitangaza siku ya leo Februari 14,kuwa ni siku kuu ya taifa na siku ya tanzia ili kuomboleza kifo cha marehemu Rafik Hariri.
Vikosi vya ulinzi vimejenga ua na kuzungusha senyenge kuwatenga wafuasi wa marehemu na wale wa upinzani waliopiga kambi kitambo sasa nje ya afisi ya waziri-mkuu Fouad Siniora tangu Desemba mosi kumshinikiza an’gatuke.
Washirika wa Hariri wanadai upinzani huo dhidi ya serikali ya Siniora unaitikia tu amri kutoka Damascus kwa lengo la kuiangusha serikali ya sasa ili kuifuta mahkama inayochunguza kesi ya mauaji siku kama leo miaka 2 iliopita ya waziri mkuu Rafik Hariri.