1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwamko wa wanawake kuhusu saratani ya kizazi ni mdogo

30 Septemba 2021

Licha ya serikali ya Tanzania kutoa bure huduma za vipimo vya awali vya saratani ya shingo ya kizazi, mwamko wa wanawake wanaopima kipimo hicho ni mdogo.

Krebs Krebszelle Illustration Symbolbild
Picha: Colourbox

Mkoa wa Mtwara pekee ulioko kusini mwa Taifa hilo, asilimia 16 ya akina mama wamegunduliwa kuwa na tatizo la saratani ya mlango wa kizazi. 

Mratibu wa huduma ya afya ya uzazi ya baba, mama na mtoto mkoa wa Mtwara Bi Rosalia Arope amefafanua kuwa katika kipindi cha Januari hadi Juni mwaka huu, akina mama 7,783 walichunguzwa na 100 walibainika kuwa na viashiria vya saratani na baada kufanyiwa uchunguzi zaidi 16 walingundulika kuwa na saratani ya shingo ya kizazi huku 43 wakionyesha kuwa na dalili kubwa za ugonjwa huo hatari.

Tumbaku inatajwa kuwa chanjo cha sarataniPicha: picture-alliance/dpa/J. Stratenschulte

Amefafanua kuwa wanawake walio kwenye hatari zaidi ni wale wenye wapenzi zaidi ya mmoja kutokana na virusi vinavyosababisha saratani ya shingo ya kizazi kubebwa na wanaume, kundi lingine ni wale walioanza tendo la kujamiana wakiwa na umri mdogo, walio zaa wakiwa na umri mdogo, walioathirika na magonjwa ya ngono, Watu wenye kinga hafifu ya mwili au magojwa kama Ukimwi, wanao zaa mara kwa mara, uzito mkubwa na kutofanya mazoezi na dalili zake zinaweza kujionyesha kuanzia miaka 10 hadi 15.

Arope anasema kwa kuwa saratani ya mlango wa kizazi ni hatari na miongoni mwa ugonjwa ambao unaondoa maisha ya wanawake wengi hapa nchini ni vyema wanawake wakajijengea utaratibu wa kufanya vipimo ambavyo ni bure katika hatua za mwanzo na kudai idadi kubwa wanaojitokeza kufanya kipimo hiko wanakuwa tayari wameshaathirika.

Malengo  ya mkoa kwa mwaka ni kuwachunguza akina mama 117,000 yani sawa  na akina 9789 kila mwezi lakini mkoa unashindwa kufikia lengo kutokana na mwamko mdogo wa wanajitokeza kupima na kufikia angalau asilimia 13 ya maadhimio.

DW, imefika katika hospitali ya wilaya ya Mtwara na kuzungumza na Hawa Malindi ambaye ni kaimu mratibu wa huduma za afya kituoni hapo, anaeleza katika halmashauri yao tatizo ni kubwa na katika kipindi cha mwezi januari hadi juni akina mama 2,309 walichunguzwa na 30 walibainika na viashiria vya saratani ya shingo ya kizazi katika awamu ya kwanza.

Katika halmashauri hiyo yenye vijiji zaidi ya 110, wahudumu wa afya wanalazimika kufanya huduma za mkoba ili kuwahamaisha na kuwafikia wanawake wengi waweze kufanyiwa vipimo vya saratani ya shingo ya kizazi kwa kuwa walio wengi wanaogopa kupima kwa kuhofia kukutwa na magonjwa ya zinaa.

Kansa ya matiti kwa wanawake ni mojawapo ya kansa inayosumbuaPicha: Imago/Chromorange

Hata hivvyo Wizara ya afya hapa nchini imeweka utaratibu wa kutoa chanjo ya saratani ya shingo ya kizazi kwa wasichana mwenye umri wa miaka 14 na kuendelea lakini mwamko wake ni mdogo kutokana na jamii kuwa na mitazamo hasi na kudhani kuwa chanjo hiyo itaharibu vizazi vya watoto wao wa kike na kupelekeaa kuwazuia kupata haki hiyo. 

Kutokana na madai ya mwamko mdogo na mitazamo hasi ambayo jamii inadaiwa kuwa nayo, DW imezungumza na baadhi ya akina mama na akina baba ili kujuwa kwa nini hawana mwamko huo wa kufuatilia hali za afya zao.

Na kuhusu suala la kuwazuia watoto wao kuchomwa chanjo ya saratani ya shingo ya kizazi wamekiri miongoni mwao kufanya hivyo kwa kuwa wamekosa elimu sahihi ya kutambua faida za chanjo hiyo.

kwa mujibu shirika la afya duniani (W.H.O) inakadiriwa kuwa asilimia 85 ya vifo vya saratani ya shingo ya kizazi hutokea katika nchi zinazoendelea. Kwa Tanzania, wastani wa wanawake zaidi ya wanawake elf 6,000 huugua saratani hiyo kila mwaka, ambapo  elf 4,355 kati yao hufa.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW