Mwana Mpotevu - Hadithi ya akinamama wanaolea watoto peke yao Barani Afrika
6 Agosti 2013Mimba za mapema mara kwa mara husababisha athari kubwa kwa mama na mtoto. Wasichana wadogo sio tu wanalazimika kukabiliana na shinikizo la kulea watoto peke yao, bali pia mara nyingi hulazimika kuacha masomo yao shuleni au chuoni. Bila elimu, mara nyingi hujikuta wakifanya kazi zenye mishahara midogo, ambazo zinashindwa kuwapa watoto wao elimu bora.
Katika mchezo huu wa redio, tunafuatilia maisha ya wasichana wawili, Kassech na Askele. Historia ya maisha yao inafanana kwani wote hawakupata elimu bora na wote bado wanaishi katika mtaa mmoja. Wasichana hawa walipata mimba za mapema na sasa wana jukumu kubwa la kuwalea watoto wao. Kassech ana tabia ya kumkaripia na kumpiga mwanawe kinyume kabisa na mwenzake Askele, ambaye licha ya kuishi maishi ya umaskini, ni mama mwenye wingi wa mapenzi kwa mtoto wake. Na hilo limemuwezesha mtoto huyo kufanya vyema shuleni. Kana kwamba hiyo haitoshi, ndugu wa kiume wa Kassech, Jonas, pia anajikuta mashakani. Mchezo huu wa redio unafuatilia kwa karibu maisha ya Kassech na jinsi anavyong’amua umuhimu wa kumpa malezi na elimu bora mtoto wake.
Mchezo huu wa redio kwa jina la ‘Mwana Mpotevu’ ni hadithi kuhusu malezi ya mzazi mmoja wa kike. Ni hadithi ya kusikitisha inayoangazia zaidi elimu ya kimsingi na jukumu la wasichana wanaojikuta katika uzazi wa mapema. Inaweka wazi hali halisi ya matatizo ya kifedha na maisha magumu wanayopitia akina mama hawa, hasa katika mataifa mengi barani Afrika. Pia inaonyesha ni vipi mtoto anavyoweza kuathirika kwa kutokuwepo mzazi wa kiume.
Noa Bongo Jenga Maisha Yako ni vipindi vinavyotayarishwa na Deutsche Welle na vinasikika katika lugha sita ikiwa ni pamoja na Kiingereza, Kiswahili, Kifaransa, Kihausa, Kireno na Kiamhara.