Mwana wa Gadaffi ahotubia taifa
21 Februari 2011Mashahidi na ripota wa shirika la habari la AFP wamesema, milio ya risasi ilizidi kusikika kufuatia hotuba iliyotolewa katika televisheni na Saif al-Islam Gaddafi.
Katika hotuba hiyo, mwana wa kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi, ameahidi mpango wa mageuzi na amesema, Baraza Kuu la Umma litakutana hii leo kujadili ajenda ya mageuzi dhahiri. Vile vile,serikali itatoa nyongeza ya mishahara.
Wakati huo huo, alionya dhidi ya hatari ya nchi hiyo kutumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe na nchi hiyo kugawika. Amekiri kuwa polisi na wanajeshi walifanya makosa walipokabiliana na waandamanaji. Lakini amepuuza ripoti kuwa mamia ya watu wameuawa.
Kwa mujibu wa makundi ya haki za binaadamu, mapamabano ya hivi karibuni nchini humo, yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 200.
Hiyo jana mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya walikutana mjini Brussels Ubeligiji, kujadili msimamo wa kuchukuliwa na umoja huo, kuhusu maandamano ya kudai mageuzi ya kidemokrasia, yaliyoibuka katika Afrika ya Kaskazini na Mashariki ya Kati.
Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton ameeleza wasiwasi wake juu ya kuongezeka kwa idadi ya waandamanaji wanaouawa kuanzia eneo la Ghuba hadi Afrika Kaskazini. Umoja wa Ulaya unahimiza uvumilivu na kukomeshwa matumizi ya nguvu dhidi ya waandamanaji.