1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwana wa Kifalme azaliwa

23 Julai 2013

Hatimae baada ya miezi tisa ya kusubiri,Kate na William wamejaaliwa kumpata mtoto wa kiume aliyekaribishwa kwa shangwe na nderemo katika taifa hilo na nje.

Kushoto ni Prince Harry,kulia ni Kate Middleton na muewe Prince William
Kushoto ni Prince Harry,kulia ni Kate Middleton na muewe Prince WilliamPicha: picture-alliance/dpa

Ama kwahakika ni furaha ya kila familia pale anapozaliwa salama salmini mtoto aliyekaa tumboni kwa mamake miezi tisa,na hivyo ndivyo ilivyo pia kwa mwanamfalme William na mkewe Kate nchini Uingereza pamoja na familia nzima ya kifalme,na umma wa taifa hilo.

Kuna shangwe katika kila kona ya taifa hilo tangu jana (22.07.2013) ambako mamia ya watu wamemiminika nje ya eneo la kasri la Buckingham kusherehekea kuzaliwa kwa mwana huyo wa kifalme.Kamera za waandishi habari wa Televisheni zilisheheni nje ya makaazi rasmi ya malkia huku umati wa watu ukifurika kujaribu kushuhudia kwa macho yao kinachoendelea katika eneo hilo punde baada ya kutangazwa kuzaliwa mtoto huyo ambaye anatajwa anaweza siku moja kutawazwa mfalme wa taifa hilo la Uingereza.

Hospitali ya St Mary's wamepiga kambi waandishi wakimsubiri KatePicha: Reuters

Kate Middleton alijifunguwa jana saa 4.24 jioni saa za Uingereza mtoto huyo akiwa na uzito wa zaidi ya kilo 3 na nusu,katika hospitali ya St Marys,Paddington ambako waandishi wa habari pia walikuwa wamepiga kambi kwa wiki tatu.Jina la mtoto huyo kwa mujibu wa wadadisi wanaofuatilia kwa karibu masuala ya familia hiyo ya kifalme bado litasalia kuwa kitendawili cha muda mrefu.

London EyePicha: Getty Images

Sherehe zilizoanza jana zinaendelea na katika maeneo ya kuvutia watalii yanatarajiwa kufurika watu wanaotaka kusherehekea uzazi huo.Aidha mara tu baada ya kutangazwa Kate amejifungua,eneo maarufu kwa watalii linalofahamika kama London Eye lililoko katikati ya jiji la London,liliwashwa taa za rangi nyekundu,nyeupe na Buluu huku jumba la BT Tower likiandikwa maandishi makubwa ya kuvutia yanayosema ''Ni mtoto wa kiume''

Wakati Kate na William wakiaanza rasmi shughuli ya malezi ambayo bila shaka inahitaji subira na uvumilivu,risala za pongezi zinaendelea pia kumiminika kutoka kila pembe ya dunia,waziri mkuu wa Ausralia,Kevin Rudd amesema yuko pamoja na familia hiyo katika wakati huu wa furaha,huko Newzealand nako shamrashamra zinaandaliwa huku maeneo 37 ya kihistoria yakitazamiwa kuwashwa taa kumkaribisha mtoto huyo wa kifalme,pongezi zimetolewa pia na waziri mkuu wa visiwa vya Solomon.

Mwandishi:Saumu Mwasimba / Reuters

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman