1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIran

Mwanadiplomasia wa Iran akutana na Mwanamfalme bin Salman

Sylvia Mwehozi
18 Agosti 2023

Waziri wa mambo ya nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian amekutana na Mwanamfalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman, wakati wa ziara yake ya kwanza nchini Saudia, tangu mataifa hayo hasimu yalipofufua uhusiano wake.

 Hossein Amir-Abdollahian- Mohammad Bin Salman
Waziri wa mambo ya nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian na Mwanamfalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman.Picha: Fars

Mwanadiplomasia huyo aliyewasili mjini Riyadh siku ya Alhamis, amefanya mazungumzo na Mwanamfalme bin Salman mjini Jeddah baada ya kurefusha ziara yake iliyokuwa awali imepangwa kuwa siku moja. Kwenye mazungumzo yao, viongozi hao wawili waligusia uhusiano wa mataifa yao na fursa za kiushirikiano pamoja na njia za kukuza uhusiano huo. Shirika la habari la Iran, IRNA limeripoti kwamba hiyo ilikuwa ni mara ya kwanza kwa afisa mwandamizi wa Tehran kukutana na Mwanamfalme bin Salman ambaye amefanya mageuzi mengi.

Soma pia: Ujumbe wa Iran wazuru Saudia kusawazisha mahusiano

Iran yenye idadi kubwa ya Waislamu wa madhehebu ya Shia na Saudia ambayo inatawaliwa na Wasunni, zilivunja mahusiano mwaka 2016 lakini zikakubaliana kuyafufua mnamo mwezi Machi kufuatia upatanishi wa China. Tangazo hilo liliibua mashaka hasa kutokana na kwamba nchi hizo mbili kubwa kikanda zinaunga mkono pande tofauti kwenye mizozo ya Mashariki ya Kati ikiwemo Yemen. Siku ya Alhamis, Amir-Abdollahian alisema kuwa uhusiano "unapiga hatua katika mwelekeo sahihi" wakati alipokutana na mwanadiplomasia mwenzake wa Saudia, Mwanamfalme Faisal bin Farhan.

Waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia Mwanamfalme Faisal bin Farhan(kulia) na mwenzake wa Iran Hossein Amir-Abdollahian .Picha: AHMED YOSRI/REUTERS

Katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari, mawaziri hao wa mambo ya nje walisema kuwa wanafanya kazi ili kuimarisha usalama na ushirikiano wa kiuchumi. Waziri Faisal alimweleza mwenzake kwamba "kurejeshwa kwa uhusiano wa kidiplomasia na Iran ni jambo muhimu kwa usalama wa kikanda".Iran na Saudi Arabia zarejesha uhusiano wa kidiplomasia

Amir-Abdollahian kwa upande wake, alipongeza ushirikiano wa kiuchumi na kiusalama kati ya nchi hizo mbili, lakini hakutangaza makubaliano mapya. Aliandamana nabalozi mpya wa Iran nchini Saudia, Alireza Enayati. "Tuna uhakika kwamba mikutano na ushirikiano huu utasaidia kuunganisha nchi za Kiislamu," alisema Amir-Abdollahian na kupendekeza "mazungumzo ya kikanda" bila kutoa maelezo. Aidha, mwanadiplomasia huyo wa Iran amegusia uwezekano wa mkutano wa wakuu wa nchi hizo mbili, ingawa hakutaja ni lini Rais wa Iran Ebrahim Raisi anaweza kusafiri hadi Saudi Arabia kwa mwaliko wa Mfalme Salman.

Tangu makubaliano ya mwezi Machi, Saudi Arabia imeongeza msukumo wa upatikanaji amani nchini Yemen, ikifanya mazungumzo ya moja kwa moja na viongozi wa Kihuthikatika mji mkuu wa Yemen Sanaa, na kutetea kurejea kwa mshirika mkuu wa Iran Syria kwenye Jumuiya ya nchi za Kiarabu. Waziri wa mambo ya nje ya Saudia Mwanamfalme Faisal alizuru Iran mnamo mwezi Juni katika ziara ya kwanza ya afisa wa ngazi ya juu kutoka taifa hilo la kifalme.

Vyanzo: dpa/afp

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW