1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwanaharakati wa Belarus apewa tuzo mbadala ya Nobel

Bruce Amani
1 Oktoba 2020

Kiongozi maarufu wa upinzani Belarus na mwanasheria wa Iran wa haki za binaadamu aliyefungwa gerezani wamepewa tuzo ya Right Livelihood, ambayo inafahamika kama "Tuzo Mbadala ya Nobel"

SPERRFRIST 01.10.2020 / 9 Uhr MESZ / Right Livelihood Awards 2020, Ales Bialiatski, Belarus
Picha: HRC Vesna/Right Livelihood Awards 2020

Wakfu wa Right Livelihood nchini Sweden unaotoa tuzo hizo, umesema unaangazia kuongezeka kwa vitisho kwa demokrasia ya ulimwengu. Ndio maana ni wakati mwafaka wa kila mmoja anayeunga mkono demokrasia kote ulimwenguni kusimama na kusaidiana. Ole von Uexkull, mkuu wa Wakfu huo amemtaja mwanaharakati wa haki za binaadamu Ales Bialiatski mwenye umri wa miaka 58 na shirika lisilo la kiserikali la Viasna ambalo analisimamia, kwa mapambano yao thabiti ya kupatikana demokrasia na haki za binaadamu nchini Belarus. "Wakati raia wa matabaka yote wakiendelea kumiminika mitaani kuupinga utawala wa kidikteta wa Rais Lukashenko,  tuzo hii kwa Bialiatski na Viasna pia ni ishara ya mshikamano wa kimataifa na wale wote wanaotafuta uhuru na demokrasia nchini Belarus"

Mwaka wa 2014 Bialiatski aliachiwa mapema baada ya kutumikia karibu miaka mitatu kabla ya kifungo chake kuisha. Alihukumiwa kwa kukwepa kulipa kodi na akapewa adhabu ya miaka minne na nusu jela mnamo Novemba 2011. Serikali za magharibi zilikosoa kesi hiyo zikisema ilichochewa kisiasa.

Bialiatski aliteuliwa kuwania tuzo ya Amani ya Nobel mwaka wa 2012 na akapata tuzo nyingi za kimataifa wakati akiwa jela. Shirika lake limetoa msaada wa kisheria kwa maelfu ya Wabelarus waliokamatwa au kufungwa jela kwa kuupinga utawala wa Rais Alexander Lukashenko.

Mwanasheria wa Iran Nasrin SotoudehPicha: Arash Ashourinia/CC0 1.0 /Right Livelihood Awards 2020

Mwanasheria wa Iran Nasrin Sotoudeh, ambaye amewatetea wanaharakati, wanasiasa wa upinzani na wanawake walioshitakiwa kwa kuvua hijab, amepewa tuzo hiyo kwa uwanaharakati wake wa kijasiri, kuyaweka maisha yake katika hatari kubwa, kukuza uhuru wa kisiasa na haki za binaadamu nchini Iran.

Mapema mwezi huu, Sotoudeh alihamishwa kutoka chumba kimoja cha jela hadi hospitali moja ya kaskazini mwa Tehran kufuatia mgomo wa kula ulioanza katikati ya Agosti.

Mwanasheria huyo mwenye umri wa miaka 58 alikamatwa 2018 kwa mashitaka ya kula njama na kuendesha propaganda dhidi ya watawala wa Iran na hatimaye akahukumiwa kifungo cha miaka 38 jela na kuchapwa viboko 158.

Wakfu huo pia umempa tuzo ya 2020 kwa Milton, mwanasheria wa haki za kiraia nchini Marekani mzaliwa wa Delaware Bryian Stevenson mwenye umri wa miaka 60 kwa kuhamasisha mabadiliko ya mfumo wa sheria ya uhalifu wa jinai nchini Marekani na kuimarisha maridhiano ya kijamii.

Mshindi wa nne ni mwanaharakati wa mazingira mwenye umri wa miaka 61 Lottie Cunningham Wren wa Nicaragua kwa kujitolea kwake kutunza mashamba ya kiasili na jamii dhidi ya unyanyasaji na uporaji.

Tuzo ya kila mwaka ya Right Livelihood ilianzishwa mwaka wa 1980 kutambua juhudi ambazo muasisi wa tuzo hiyo, mfadhili wa Sweden mwenye asili ya Ujerumani Jakob von Uexkull, anahisi kuwa zinapuuzwa na tuzo za Nobel.

dpa, ap