1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwanajeshi wa Marekani na Uingereza wauawa nchi Iraq

Babu Abdalla12 Machi 2020

Wanasiasa wa ngazi ya juu nchini Iraq wameungana na Umoja wa Mataifa kulaani vikali shambulio la roketi kaskazini mwa Baghdad lililowaua raia wawili wa Marekani na mwanajeshi wa Uingereza.

Irak Ausbildung Soldaten durch US Militär
Picha: picture-alliance/dpa/K. Al-A'nei

Jumla ya makombora 18 ya roketi yalirushwa katika kambi ya Taji, na kumuua mwanajeshi mmoja wa Uingereza na mwengine wa Marekani pamoja na mkandarasi wa Marekani.

Shambulio hilo limechukuliwa kuwa shambulizi baya zaidi dhidi ya vikosi vya jeshi la Marekani vinavyohudumu nchini Iraq katika miaka ya hivi karibuni.

Katika shambulio hilo, hakuna kundi lolote ambalo limejitokeza na kudai kuhusika, lakini Marekani imewanyooshea kidole cha lawama kundi la wapiganaji la Iraq la Hashed al-Shaabi.

Yumkini baada ya saa chache tu ya shambulizi hilo, wapiganaji 26 wa kundi la Hashed al-Shaabi waliuawa katika shambulizi la anga katika mkoa wa al-Bou mashariki mwa Syria, hatua ambayo inaonekana kuwa ya kulipiza kisasi.

Inahofiwa kuwa hali hiyo huenda ikaongeza vuta nikuvute kati ya Marekani na Iran.

Mkuu wa shirika la kutetea haki za binadamu la Syria Rami Abdel-Rahman ameliambia shirika la habari la DPA kuwa: "Nadhani ndege zinazoongozwa na wanajeshi wa muungano wa Marekani zimeishambulia kambi ya wapiganaji hao kama njia ya kulipiza kisasi kwa shambulio la mapema lililofanywa katika kambi ya Taji."

Shirika hilo limesema kuwa mashambulizi 10 ya anga yamefanywa na ndege tatu tofauti zilizowalenga wapiganaji hao wanaoungwa mkono na Iran katika eneo la Boukamal, mashariki mwa Syria karibu na mpaka wa Iraq.

Mwanajeshi wa Marekani akiwafundisha wanajeshi wa Iraq jinsi ya kutumia bunduki Picha: picture-alliance/dpa/A. Al-Shemaree

Hata hivyo, maafisa wa Marekani wamesema kuwa shambulio hilo halihusiani kabisa na shambulio lililofanywa katika kambi ya Taji. Haijabainika wazi ni nani aliyehusika na shambulio hilo.

Alhamisi (12.03.2020), kamanda wa jeshi la Iraq amesema kuwa shambulio hilo ni changamoto kubwa ya usalama na ameahidi kufanya uchunguzi.

Naye Rais Barham Saleh na spika wa bunge la Iraq Mohammed al-Halbussi pia wamelaani shambulio hilo.

Kupitia taarifa, Ujumbe wa Umoja wa mataifa nchini Iraq umetoa wito kwa pande zote kujizuia kuchukua hatua zaidi.

Aidha, ofisi za wanadiplomasia wa Marekani zimekuwa zikishambuliwa pamoja na kambi za jeshi la Marekani. Marekani ina wanajeshi 5200 wanaohudumu nchini Iraq.

 

 

Vyanzo DPA/AFP/AP

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW