1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwanamfalme bin Salman aizuru Uturuki

22 Juni 2022

Mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman amewasili Ankara Jumatano akifanya ziara yake ya kwanza Uturuki tangu alipouliwa mwandishi wa habari wa Saudia Jamal Khashoggi katika ubalozi mdogo wa Saudia Istanbul.

Saudi-Arabien Besuch Präsident Erdogan bei Mohammed bin Salman
Picha: MURAT C. MUHURDAR/Turkish Presidency/AFP

Rais Reccep Tayyip Erdogan wa Uturuki amempokea mwanamfalme huyo katika kasri lake la rais na kisha atakula naye chakula cha jioni baadae. Hakujapangwa kikao chochote na waandishi wa habari kufuatia kuwasili kwa kiongozi huyo.

Mazungumzo ya viongozi hao wawili mjini Ankara yanakuja mwezi mmoja kabla ziara ya Rais wa Marekani Joe Biden mjini Riyadh ambapo atahudhuria mkutano wa kilele utakaojikita katika mzozo wa nishati uliotokana na Urusi kuivamia Ukraine.

Hali ya maisha Uturuki inazidi kuwa ngumu kuelekea uchaguzi mkuu

Uamuzi wa Erdogan wa kufufua mahusiano na mmoja wa mahasimu wakubwa wa Uturuki,Saudi Arabia, unatokana na masuala ya kiuchumi na kibiashara. Kiongozi huyo wa Uturuki amesema mazungumzo yao yatalenga kuupeekea uhusiano wa nchi hizo mbili kufikia kiwango cha juu zaidi.

Saudia yazidi kushinikizwa kuhusu Khashoggi

01:19

This browser does not support the video element.

Erdogan aliitembelea Saudi Arabia mwezi Aprili, hiyo ikiwa ziara yake ya kwanza katika nchi hiyo ya kifalme tangu mwaka 2017, mwaka mmoja kabla mauaji ya kikatili ya Jamal Khashoggi.

Serikali ya Erdogan ilitoa taarifa chache mno kuhusiana na mauaji hayo yaliyomuaibisha pakubwa mwanamfalme Mohammed bin Salman ambaye huko uturuki yuko katika hatua ya mwisho ya ziara yake ya Mashariki ya kati ambapo amezitembelea pia nchi za Misri na Jordan.

Wachambuzi wanaamini kwamba mwanamfalme huyo anataka kuona iwapo atapata uungwaji mkono mkubwa kuelekea maelewano mapya ya makubaliano ya nyuklia kati ya nchi zenye nguvu duniani na hasimu wa Saudi Arabia, Iran.

Hali ya maisha ya Waturuki inazidi kuwa ngumu mwaka mmoja kabla uchaguzi mkuu ambao unampa mojawapo ya changamoto kubwa zaidi alizowahi kukumbana nazo katika utawala wake wa miongo miwili.

Mahusiano ya kidiplomasia hayawezi kuhalalisha ukosefu wa haki

Ziara hii inafanyika wakati ambapo mpenzi wa Khashoggi alisema Jumatano kuwa uhalali wa kisiasa anaopokea mwanamfalme bin Salman kila anapofanya ziara katika nchi zengine, haubadilishi hoja ya kwamba yeye ni "muuaji."

Mpenzi wa Khashoggi, Hatice CengizPicha: Isa Terli/AA/picture alliance

Mpenzi huyo wa Khashoggi ambaye ni raia wa Uturuki, Hatice Cengiz, aliandika kwenye ukurasa wa mtandao wake wa kijamii wa Twitter kwamba ziara ya Mohammed bin Salman Uturuki haibadilishi hoja ya kuwa alihusika katika mauaji.

Cengiz alisema hayupo na Khashoggi tena ila vita vya kupata haki si vita vyake pekeyake bali ni vita vya kila mtu aliye huru na mwenye kufikiria. Aliongeza kwamba hakuna mahusiano yoyote ya kidiplomasia yanayoweza kuhalalisha ukosefu huu wa usawa na haki.

Saudi Arabia imejaribu kupanua ushirikiano wake na mataifa mbalimbali wakati ambapo mahusiano yake na Marekani yameharibika.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW