1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwanamfalme Charles asikitishwa na utumwa

24 Juni 2022

Mkutano wa kilele wa viongozi wa Jumuiya ya Madola mjini Kigali, Rwanda viongozi wamesema nchi zilizoendelea hazipaswi kulikimbia jukumu lao la kuzisaidia nchi zinazoendelea kutokana na matatizo yanayozikabili.

Deutschland | Volkstrauertag | Prinz Charles spricht im Bundestag
Picha: Axel Schmidt/AFP

Kupitia hotuba za viongozi waliozungumza leo katika mwanzo wa kikao hiki cha siku mbili, Jumuiya ya Madola bado inakabiliwa na changamoto kadhaa kwenye nyanja za demokrasia, ustawi wa jamii, sheria, athari za uharibifu wa mazingira na usawa wa kijinsia katika jamii. Haya yote yamekuwa kiini cha hotuba ya kila kiongozi aliyezungumza.

soma Mkutano wa kilele wa Jumuiya ya madola umefunguliwa rasmi mjini Kigali

Rais wa Rwanda Paul Kagame, ambaye ni mwenyeji wa mkutano huu wa kilele amewaeleza viongozi wenzake kwamba nchi katika Jumuiya ya Madola na katika ulimwengu mwingine zinakabiliwa na matatizo kadhaa na Jumuiya ya Madola haipaswi kukaa kando bila kutafuta suluhu la matatizo hayo.

''Jumuiya ya Madola tunayoihitaji ni ile inasimama mstari wa mbele kutatua changamoto za ulimwengu, si ile inayokaa pembeni kama mtazamaji wakati wa matatizo yakitokea. Nguvu zetu pamoja ni kuweka mambo sawa ambayo vinginevyo yangekuwa hayapewi umuhimu.''

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola Patricia Scotland yeye amesema kwamba jumuiya hii inatakiwa kuchukua mwelekeo mpya ili kukabiliana na changamoto za ulimwengu wa leo tofauti na ilivyokuwa wakati jumuiya hii ilipoundwa mwaka 1926

''Misukosuko ya vita na usalama mdogo kwenye ulimwengu wetu, kupanda kwa bei ya vyakula na mafuta na mtikisiko wa kiuchumi haya yote yanatishia kuleta hali ya mgogoro mzito. Mkutano huu kwa hiyo ni fursa muhimu ya kutafuta suluhu la matatizo haya.''

Mapendekezo

Picha: Dan Kitwood/ASSOCIATED PRESS/picture alliance

Moja ya suluhu hilo ni pendekezo ambalo limekuwepo kwa miaka mingi la kuzitaka nchi zilizoendelea na zilizoko kwenye jumuiya ya madola kusaidia kwa hali na mali kutatua changamoto zinazokabili zinazoendelea.

Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson akizungumza amesema Uingereza inalitambua na ndiyo kuanzia mwaka 2018 imechukua mikakati.

''Katika mkutano wa Jumuiya ya Madola mjini London mwaka 2018, serikali ya Uingereza ilitangaza pauni milioni 2012 za kusaidia elimu ya mtoto wa kike katika nchi maskini kwenye jumuiya yetu na ninafurahi kusema kwamba hadi sasa mkakati huu unaendelea kutekelezwa katika nchi 11 ili kuhakikisha wasichana wote wanapata elimu bora angalau hadi miaka 12.'

soma Uingereza yalaani uamuzi wa kuzuia waomba hifadhi kupelekwa Rwanda

Lakini Mwanamfalme Charles ambaye anamuwakilisha Malkia Elizabeth wa Uingereza amesema, ''Kufanya kazi pamoja tunajenga urafiki wa kudumu na niseme wazi kwamba ninavyoona mimi naona kuna masomo ya kuchukua kutoka jumuiya hii ya madola, wakati tunajitahidi kuboresha uhusiano na kutatua changamoto napenda niseme kwamba vyanzo vya baadhi ya matatizo vinaanzia enzi za ukoloni na ikiwa tunataka kupiga hatua nzuri ni lazima baadhi yetu mchango wetu katika matatizo haya.''

Mkutano huu wa kilele wa wakuu wa nchi na serikali unatazamiwa kukamilikaa kesho Jumamosi, lakini Mwanamfalme Charles yeye ataondoka usiku huu kurudi London.

 

Sylvanus Karemera 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW