1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwanamfalme Philip afariki na miaka 99

9 Aprili 2021

Viongozi mbalimbali ulimwenguni wanaendelea kutuma salamu za rambirambi kwa Malkia Elizabeth wa II wa Uingereza kufuatia kifo cha mumewe Mwanamfalme Philip, aliyefariki dunia leo akiwa na umri wa miaka 99. 

England I Prinz Philip I The Duke of Edinburgh
Picha: Nigel Treblin/Getty Images

Tangazo kutoka Kasri la Buckingham lilisema Mwanamfalme Philip alifariki dunia mapema leo kwa amani katika Makazi ya Kifalme ya Windsor.

Bendera zilipepea nusu mlingoti kwenye majengo ya kifalme na ya serikali na tangazo la kifo chake kubandikwa kwenye lango la Kasri la Buckingham. Soma zaidi Mwanamfalme Philipp ameaga Dunia

Kifo cha Philip ni pigo kwa Malkia Elizabeth wa II wa Uingereza mwenye umri wa miaka miaka 94, ambaye wakati mmoja alimuelezea ”kuwa mtu anayempa nguvu maishani mwake”

Kamanda huyo wa zamani wa jeshi la wanamaji aliitumia nafasi yake ya kuwa mume wa malkia kwa kusaidia katika shughuli za hisani. Alilazwa katika hospitali Februari 16, na akaenda nyumbani baada ya mwezi mmoja ambapo alitibiwa tatizo la moyo lililomsumbua kwa muda mrefu

Mwanamfalme Philip na Malkia ElizabethPicha: Keystone/Zuma/Imago Images

Viongozi mashuhuri duniani wa sasa na waliostaafu wanaendelea kutoa salamu zao za rambirambi, wakimwelezea marehemu kama mtu aliyeutumikia Ufalme wa Uingereza kwa juhudi na uadilifu. Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson amesema Hayati Philip alijipatia heshima kubwa nchini Uingereza, katika Jumuiya ya Madola na kwingineko duniani. Kiongozi wa chama cha upinzani cha Labour, Keir Starmer, amesifu huduma ya miongo mingi ya Mwanamfalme Philip kwa Uingereza, kwanza kama mwanajeshi katika kikosi cha wanamaji, na kisha kama mume wa Malkia kwa zaidi ya miaka 70. Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Heiko Maas, amesema Ujerumani imehuzunishwa na kifo cha Mwanamfalme Philip.

Picha: PA/AP/picture alliance

Mkuu wa Halmashauri Kuu ya Ulaya Ursula von der Leyen amesema amehuzunishwa na habari za kifo cha mwanamfalme wa Uingereza Philip na akatuma rambirambi zake kwa Malkia Elizabeth na watu wa Uingereza.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alimuelezea Philip kuwa mtumishi wa umma mkamilifu na atakumbukwa sana Israel na kote duniani. 

Rais wa zamani wa Marekani George W Bush alisema Philip aliiwakilisha nchi yake na heshima.

Philip alistaafu kutoka majukumu ya umma mwaka wa 2017 akiwa na umri wa miaka 96. Kifo chake kimekuja miezi michache tu kabla ya kusherehekea 100 ya kuzaliwa kwake Juni – hafla ambayo kawaida huadhimishwa Uingereza kwa ujumbe wa salamu za pongezi kutoka kwa malkia, ambaye sasa ndiye mtawala wa kifalme aliyehudumu kwa muda mrefu Zaidi Uingereza.

Philip na Elizabeth walifunga ndoa katika kanisa maarufu la Westminster Abbey mjini London mnamo mwaka wa 1947.     

     

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/AP/Reuters

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW