Mpango wa nyuklia wa Iran uko matatani
20 Machi 2018Saudi Arabia ni mmoja wa washirika wakubwa wa Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati wakati nchi hizo mbili zikiiangalia Iran kama kitisho cha usalama. Viongozi hao wawili, Mwanamfalme Mohammed Bin Salman na Rais Donald Trump, wanatarajiwa kuzungumzia mgogoro wa Yemen, mpango wa kuubadilisha uchumi wa Saudi Arabia kutoka utegemezi wa mafuta pekee na pia suala la haki za wanawake.
Katika mpango huo wa kuzindua mabadiliko ya kiuchumi chini ya Dira 2030, Mwana Mfalme Mohammed aliye na miaka 32 atakuwa anatafuta uungwaji mkono wa kisiasa na uwekezaji kutoka Marekani. Kando na mazungumzo yake na Trump, Mwana Mfalme Salman pia atakutana na maafisa mbalimbali wa Marekani walio na ushawishi akiwemo Waziri wa Ulinzi, Hazina na Biashara pamoja na wakuu wa shirika la ujasusi, CIA.
Katika suala la vita vya Yemen, Marekani inaunga mkono muungano unaoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya waasi wa Kihouthi wanaoungwa mkono na Iran. Vikosi vyake vimevisaidia vile vya Saudia kwa kujaza mafuta ndege zao za kivita angani, kuwapa silaha na kutoa taarifa za kijasusi. Lakini kumekuwa na ukosoaji katika bunge la Marekani juu ya usaidizi huo wa kijeshi huku bunge la Seneti likitarajiwa kupiga kura wiki hii, juu ya azimio la pamoja la kumtolea wito Trump kusimamisha msaada huo.
Katika mahojiano na kituo cha habari cha Marekani, CBS, yaliyorushwa hewani siku ya Jumapili, Mwana Mfalme Bin Salman alitetea hatua ya taifa lake katika vita vya Yemen akidai Yemen imetawaliwa na itikadi za Iran.
Kwenye siasa za ndani, Bi Salman alisema kuwa sasa nchi yake inapambana na rushwa, na kufanya kazi ili kurekebisha makosa ya uvunjifu wa haki za binaadamu.
Mpango wa nyuklia wa Iran uko matatani
Kuhusiana na mpango wa nyuklia wa Iran, Saudi Arabia imeyataja makubaliano ya kihistoria kati ya Iran na nchi zenye nguvu zaidi duniani yaliyofikiwa mwaka 2015 kuwa yana mapungufu. Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, Adel al-Jubeil, amewaambia waandishi habari mjini Washington mtizamo wao ni kuwa makubaliano hayo yana mapungufu.
Awali Trump alitishia kuyavunjwa makubaliano hayo isipokuwa pakiwepo na mabadiliko ifikapo mwezi Mei. Wiki iliyopita rais huyo wa Marekani alimfuta kazi waziri wake wa amabo ya nchi za nje, Rex Tillerson, baada ya kuonekana kuyatetea na kumchagua Mike Pompeo ambaye ni mkurugenzi wa sasa wa CIA na mkosoaji wa mpango huo kuchukuwa nafasi ya Tillerson.
Hii itakuwa ni ziara ya pili ya Mwana Mfalme Salman katika ikulu ya Marekani tangu Rais Trump aingie madarakani na ziara ya kwanza tangu alipotangazwa kuwa mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia. Viongozi hao wawili walikutana mjini Riyadh wakati Trump alipoizuru Saudi Arabia mwezi Mei mwaka huu.
Mwandishi: Amina Abubakar/dpa/AP
Mhariri: Mohammed Khelef