1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi ya Tanzania yamtia mbaroni Dk.Wilbroad Slaa

Admin.WagnerD14 Agosti 2023

Mwanasiasa mkongwe nchini Tanzania, Dokta Wilbroad Slaa anashikiliwa na jeshi la polisi nchini humo akikabiliwa na makosa ya uhaini.

Tansania | Hafen in Dar es Salaam
Picha: Xinhua/picture alliance

Hayo yanajiri ikiwa ni siku chache tangu, Mkuu wa Jeshi la polisi, IGP Camilius Wambura, kutamka kuwa kuna Watanzania wenye nia ya kumpindua Rais Samia Suluhu Hassan.

Dk Wilbroad Slaa ambae aliwahi kuwa Balozi wa Tanzania, nchini Sweden, na nwanasiasa mashuhuri amekamatwa nyumbani kwake Mbweni, jijini Dar es Salaam akikabiliwa na makosa ya uhaini.

Mahali alipo Dokta Slaa.

Mkuu wa Jeshi la Polisi, nchini Tanzana, IGP Cammilius Wambura akizungumza na Deo Kaji wa DWPicha: Deo Kaji Makomba/DW

Akizungumza na DW Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi, Jumanne Muliro, amekiri kua jeshi hilo linamshikilia Dr Slaa lakini akaahidi kueleza kwa kina baadaye.

Wakati huo huo,  Wakili wa Dr Slaa, Dickson Matata, amesema mwanadiplomasia huyo alikamatwa jana mchana na akapelekwa kituo cha polisi cha Mbweni, jijini hapa na baadaye polisi walikwenda kumpekua nyumbani kwake majira ya saa 8 mchana.

Kwa mujibu wa Wakili Matata, Dk Slaa alipelekwa kituo cha polisi cha Oysterbay ambako alihojiwa kwa makosa ya uchochezi lakini wakati wakiwa katikati ya mahojiano hayo, kesi ilibadilishwa na kuwa ya uhaini.

Polisi: Yeyote anaeanzisha vita dhidi ya jamhuri ana kosa la uhaini.

Kwa mujibu wa katiba ya Tanzania, mtu yeyote  aliye ndani ya nchi na kuanzisha vita dhidi ya Jamhuri ya Muungano,atakuwa na hatia ya kosa la uhaini na atawajibika kwa adhabu ya kifo na kosa hilo halina dhamana.

Pamoja na Dk Slaa Wengine waliokamatwa ni Wakili Boniface Mwabukusi na mfuasi wa Chadema Mdude Nyagali, ambao  wamekuwa wakiupinga mkataba wa uwekezaji kati ya  bandari ya Tanzania na kampuni ya DP World ya Dubai.

Akizungumzia kamatakamata hiyo, Askofu Mkuu wa Kanisa la Moravian, Tanzania, Emmaus B Mwamakula amesema kinachoonekana wanaopinga mkataba wa bandari wanabambikiwa kesi ili kuwanyamazisha.

Soma zaidi;Mahakama Kuu Tanzania yabariki mkataba wa bandari

Agosti 10 mwaka huu, mahakama kuu kanda ya Mbeya, ilitupilia mbali kesi iliyofunguliwa na mawakili wanne, wakiupinga mkataba wa bandari na kampuni ya DP World ya Dubai. Saa chache baadaye, Mkuu wa Jeshi la Polisi, nchini Tanzana, IGP Cammilius Wambura, alitangaza na kuwaonya wenye mipango ya kumpindua, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

DW: Dar es Salaam

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW