Mwanasiasa Steinbach ajitoa chama cha CDU
16 Januari 2017Kuhusu mada ya kujitoa katika chama cha Christian Democratic Union, CDU kwa mwanasiasa Erika Steinbach akipinga sera za wakimbizi za kansela Merkel gazeti la Stuttgarter Zeitung liliandika:
Si lazima mtu awe mtume ili kuweza kusema kwamba kujitoa kwa Steinbach kutoka chama cha Christian Democratic Union, CDU, ni sawa na kujitafutia umaarufu miongoni mwa wafuasia wa kihafidhina wa siasa kali za mrengo wa kulia na sio hatua ya mwisho ya kukipatia silaha chama mbadala wa Ujerumani, AfD, ambacho tayari kilijaribu kumvutia Steinbach kuwa mwanachama wake baada ya kuvunjwa moyo na sera za kihadhina. Jina la Steinbach litaendelea kusikika mara kwa mara katika mpambano wa kuwania uchaguzi wa Ujerumani, lakini mhariri anasisitiza kwamba sio katika chama cha CDU.
Katika mada hiyo hiyo gazeti la Nordwest-Zeitung kutoka Oldenburg mhariri anaandika kwamba baada ya Steinbach kujitoa chama cha CDU hakuna shaka tena kwamba wahafidhina nchini Ujerumani hawana tena makaazi. Mhariri alieendelea kuandika kwamba mtu anatambua hilo kutokana na msingi kwamba tangu wakati wa mjadala wa kuelekea mrengo wa kushoto mwaka 2010, Steinbach hakuweza kuficha tena msimamo wake. Matakwa yake ni kuelemea mrengo wa kulia zaidi na ndio msimamo wake kuhusu demokrasia. Kansela pamoja na chama chake lakini katika miaka iliyopita wamevunja sheria hiyo muhimu. Baada ya hatua ya kuiokoa sarafu ya euro, kuliingia mzozo wa wakimbizi. Ndio sababu wakati mhafidhina kama Steinbach amezungumzia masuala hayo wakati akitoa maelezo juu ya kujitoa kutoka katika chama hicho.
Amani ya Mashariki ya Kati
Mada nyingine katika magazeti ni kuhusu mkutano wa amani ya mashariki ya kati uliofanyika mjini Paris nchini Ufaransa.
Mhariri aliandika - Ufaransa iliyaalika mataifa 70 ambayo yalituma mawaziri wake wa mambo ya kigeni ama wawakilishi wengine katika mkutano na matarajio yake ni kuimarisha amani katika mashariki ya kati. Lakini kulikuwa na hali ya kukatisha tamaa katika mkutano huo. Msimamo wa suluhisho la mataifa mawili unaporomoka, kulikuwa na hamasa lakini, kwa hali halisi, ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi katika eneo la ukingo wa magharibi, hatua ya Israel kuyumbisha mazungumzo, na tatizo ambalo halijapatiwa ufumbuzi la Ukanda wa Gaza, yote hayo hayajabadilika. Wasiwasi umetanda kimataifa kuhusu suala hili, hususan kutokana na ujumbe wa rais mteule wa Marekani Donald Trump kabla ya kuingia katika ikulu ya Marekani, White House.
Taarifa za uwongo
Kuhusiana na suala la taarifa za uwongo katika mtandano wa kijamii wa Facebook mhariri wa gazeti la Frankfurter Rundschau aliandika: Kampuni ya Facebook kwa muda wa mwezi mzima haikuchukua hatua yoyote kuhusu athari, kuhusiana na suala la taarifa bandia. Sasa Facebook imezungumza dhidi ya taarifa hizo bandia. Huo ni uamuzi ambao umechelewa mno. Ni muda mrefu sana umepita ambapo kumekuwa na taarifa hizi chafu za kihalifu. Mhariri alisisitiza kwamba muda umefika kwa facebook kutambua wajibu wake kabla ya uchaguzi mkuu nchini Ujerumani.
Mwandishi : Sekione Kitojo / Inlandspresse
Mhariri: Idd Ssessanga