1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kada wa upinzani 'alietekwa' Tanzania akutwa amekufa

9 Septemba 2024

Mwanachama wa chamakikuu cha upinzani nchini Tanzania, CHADEMA, Ali Mohamed Kibao amekutwa amekufa baada ya kutekwa, kupigwa na kumuagiwa tindikali, amesema kiongozi wa chama hicho Freeman Mbowe siku ya Jumapili.

Marehemu Ali Mohamed Kibao
Marehemu Ali Mohamed KibaoPicha: Chadema

Maafisa wa CHADEMA wamesema Ali Mohamed Kibao, mjumbe wa kamati ya taifa ya Chadema, alilaazimishwa kushuka kwenye basi kwa mtutu wa bunduki siku ya Ijumaa na wanaoshukiwa kuwa maafisa wa usalama wakati akisafiri kutoka Dar es Salaam kwenda mji wa bandari wa kaskazini wa Tanga.

Mwili wake ulikutwa katika eneo la Ununio, mkoa wa Dar es Salaam Jumamosi usiku, tukio hilo likijiri chini ya mwezi ya mmoja baada ya Mbowe, naibu wake Tundu Lissu na viongozi wengine wa Chadema, kukamatwa katika hali iliyoibua wasiwasi kuhusu kupungua kwa nafasi ya kidemokrasia nchini Tanzania.

Soma pia: Tanzania: Visa vya mauaji na watu wasiojulikana katika eneo la Matevesi mkoani Arusha

"Uchunguzi wa maiti umefanywa (na kushuhudiwa na) mawakili wa Chadema na ni wazi kuwa Kibao alipigwa sana na kumwagiwa tindikali usoni,” Mbowe aliwaambia waandishi wa habari.

"Hatuwezi kuruhusu watu wetu waendelee kutoweka au kuuawa hivi," alisema. "Maisha ya viongozi wa Chadema kwa sasa yako hatarini."

Alisema maafisa wengine kadhaa wa chama pia walipotea, bila kutoa maelezo.

Mahojiano maalum ya DW na rais Samia Suluhu Hassan

20:47

This browser does not support the video element.

Rais Samia aagiza uchunguzi wa kina na majibu ya haraka

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alisema amepokea taarifa za mauaji ya Kibao "kwa masikitiko makubwa" na akatoa salamu za rambirambi kwa familia yake, marafiki na viongozi wa chama.

"Nimeagiza mamlaka za uchunguzi kunipa ripoti ya kina juu ya tukio hili baya sana na kesi kama hizo haraka," alisema katika chapisho kwenye X, zamani Twitter.

"Nchi yetu ni ya kidemokrasia, na kila raia ana haki ya kuishi. Serikali ninayoiongoza haitavumilia vitendo hivyo vya kikatili."

Soma pia: Rais Samia ampa Simba jina la Tundu Lissu

Kibao alikuwa ofisa mstaafu wa upelelezi wa kijeshi aliyewahi kufanya kazi na vyama vingine vya upinzani pamoja na Chama tawala (CCM) kabla ya kujiunga na Chadema.

Mkurugenzi wa Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema aliliambia shirika la habari la AFP kuwa Kibao ana umri wa miaka 69 na amekuwa mwanachama wa chama hicho tangu mwaka 2008.

Polisi ilisema katika taarifa kuwa inaendelea kuchunguza "tukio hili la kusikitisha" na kuapa kwamba waliohusika watafikishwa mahakamani.

Hofu ya kurejea kwa sera za udhalimu

Mashirika ya kutetea haki za binadamu na wapinzani wa serikali yameelezea hofu kuwa ukandamizaji wa hivi karibuni dhidi ya upinzani unaweza kuashiria kurejea kwa sera dhalimu za mtangulizi wa Samia, hayati rais John Magufuli.

Tundu Lissu: Siwezi kusema ninao uhakika wa usalama wangu

03:24

This browser does not support the video element.

Kukamatwa huko kulikuja licha ya Samia kuahidi kurejea katika "siasa za ushindani" na kupunguza vikwazo kwa upinzani na vyombo vya habari, ikiwa ni pamoja na kuondoa marufuku ya miaka sita ya mikusanyiko ya upinzani.

Soma pia: Mbowe: Tunataka tume itayochunguza visa vya utekaji Tanzania

Amnesty International ilisema kukamatwa kwa watu wengi mwezi Agosti ni "ishara ya kutia wasiwasi sana" katikati mwa maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa mwezi Desemba 2024 na uchaguzi mkuu mwishoni mwa mwaka ujao.

Mbowe mwenyewe pia alikamatwa Julai 2021 kabla ya mkutano wa chama kudai marekebisho ya katiba kabla ya kuachiliwa Machi iliyofuata baada ya waendesha mashtaka kufuta mashtaka ya ugaidi dhidi yake.

Lissu, ambaye aligombea urais bila mafanikio mwaka 2020, pia amekamatwa mara nyingi na alinusurika jaribio la mauaji mwaka 2017.

Alirejea Tanzania, baada ya kuishi uhamishoni kwa zaidi ya miaka mitano, kufuatia uamuzi wa Samia wa mwaka 2023 kuondoa marufuku dhidi ya upinzani.