1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwanasiasa wa upinzani wa Senegal Ousmane Sonko akamatwa

Sylvia Mwehozi
29 Julai 2023

Mwanasiasa mkuu wa upinzani wa Senegal Ousmane Sonko amekamatwa jana baada ya kuvutana na maafisa wa usalama waliokuwa wamezingira makaazi yake.

Senegal - Ousmane Sonko
Mwanasiasa mkuu wa upinzani wa Senegal Ousmane Sonko Picha: Seyllou/AFP

Mwanasiasa mkuu wa upinzani wa Senegal Ousmane Sonko amekamatwa jana baada ya kuvutana na maafisa wa usalama waliokuwa wamezingira makaazi yake. Awali Sonko mwenye umri wa miaka 49, aliandika kupitia mtandao wa X, zamani ukijulikana kama Twitter, kwamba wanajeshi walimchukua video kwa kutumia simu zao wakati alipokuwa akirejea kutoka Msikitini na hivyo kusababisha purukushani baina yake na maafisa wa usalama aliowataka kufuta video zake.

Sonko alihukumiwa adhabu ya kifungo cha miaka miwili jela mnamo mwezi Juni, katika hukumu iliyozua maandamano makubwa ya vurugu. Hukumu hiyo ilitia shaka uwezo wake wa kuwania urais katika uchaguzi wa mwaka ujao.

Mwanasiasa huyo alisusia kesi mahakamani na kusalia nyumbani kwake mjini Dakar tangu uamuzi huo, akisema vikosi vya usalama vilivyokuwa nje ya nyumba yake vinamzuia kuondoka.