1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UhalifuUlaya

Mwanaume wa Kifaransa akiri "mimi ni mbakaji"

17 Septemba 2024

Mwanaume mmoja nchini Ufaransa amekiri kumlisha mke wake madawa ya kulevya na kuwaalika wanaume kadhaa kumbaka. Anatuhumiwa pia kwa ukiukaji kadhaa wa faragha kwa kurekodi na kusambaza picha na ngono.

Mashtaka ya udhalilishaji Avignon
Dominique Pelicot na washukiwa wengine 50 wanaoshtakiwa mjini Avignon wanakabiliwa na kifungo cha hadi miaka 20 gerezani kila moja.Picha: Manon Cruz/REUTERS

Mwanamume wa Kifaransa mwenye umri wa miaka 71 amekiri mahakamani Jumanne kwamba alimnywesha mke wake wa wakati huo dawa za kulevya na kuwaalika wanaume kadhaa kumbaka kwa takriban muongo mmoja, pamoja na kumbaka yeye mwenyewe. Alimuomba yeye, na watoto wao watatu, msamaha.

"Leo nasisitiza kwamba, pamoja na wanaume wengine hapa, mimi ni mbakaji", Dominique Pélicot aliiambia mahakama. "Walijua kila kitu. Hawawezi kusema vinginevyo."

Ushahidi wa Dominique Pélicot ndio wakati muhimu zaidi kufikia sasa katika kesi ambayo imeshtua na kushika nchi, na kuongeza ufahamu mpya kuhusu unyanyasaji wa kingono. Wengi pia wanatumaini ushuhuda wake utatoa mwanga - kujaribu kuelewa mambo yasiyofikirika.

Ingawa hapo awali alikiri kwa wachunguzi, ushahidi wa mahakama utakuwa muhimu kwa jopo la majaji kuamua juu ya hatima ya wanaume wengine 50 wanaoshtakiwa pamoja naye.

Wengi wanakanusha kumbaka Gisèle Pélicot, wakisema walilaghaiwa na mume wake wa wakati huo au kudai waliamini kuwa alikuwa akiridhia.

Muathirika amulika mapambano dhidi ya unyanyasaji

Gisèle Pélicot amekuwa ishara ya mapambano dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia nchini Ufaransa kwa kukubali kujitokeza wazi katika kesi hiyo, kuruhusu kesi hiyo kusikizwa hadharani, na kuonekana wazi mbele ya vyombo vya habari.

Anatarajiwa kuongea mahakamani baada ya mume wake wa zamani kutoa ushahidi siku ya Jumanne. Chini ya sheria ya Ufaransa, kesi ndani ya chumba cha mahakama haiwezi kurekodiwa au kupigwa picha.

Wakili wa Mfaransa aliyekiri kushtakiwa kwa makosa ya jinai katika kesi iliyovutia hisia sana ya ubakaji akizungumza na vyombo vya habari.Picha: Christophe Simon/AFP/Getty Images

Dominique Pélicot anafikishwa mahakamani kupitia lango maalum lisiloweza kufikiwa na vyombo vya habari, kwa sababu yeye na washtakiwa wengine wanazuiliwa wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo.

Soma pia: Siasa za Ufaransa zatikiswa na kesi ya ubakaji dhidi ya Strauss-Kahn

Washtakiwa ambao hawako rumande huja kwenye kesi hiyo wakiwa wamevaa barakoa au kufunika nyuso zao ili kuepuka kurekodiwa au kupigwa picha nyuso zao.

Baada ya siku kadhaa za kutokuwa na uhakika kutokana na hali yake ya kiafya, Dominique Pélicot alifika mahakamani Jumanne na kuwaambia majaji kwamba anakiri mashtaka dhidi yake.

Ushuhuda wake uliokuwa ukingojewa sana ulicheleweshwa kwa siku kadhaa baada ya kuugua, akiwa na jiwe kwenye figo na maambukizi ya mkojo, mawakili wake walisema.

Alifanya alichofanyiwa na kufanyishwa akiwa mdogo

Akiwa ameketi kwenye kiti cha magurudumu, Pélicot alizungumza na mahakama kwa saa moja, kuanzia maisha yake ya utotoni hadi miaka ya unyanyasaji dhidi ya mke wake wa zamani.

Akionyesha majuto, sauti yake ikitetemeka na nyakati fulani haisikiki, alijaribu kueleza matukio ambayo alisema yalimtia kovu utotoni na kupanda mbegu ya uovu ndani yake.

"Mtu hazaliwi akiwa mpotovu, anageuka mpotovu," Pélicot aliwaambia majaji, baada ya kusimulia, wakati mwingine kwa machozi, kubakwa na mwanaume muuguzi hospitalini alipokuwa na umri wa miaka 9 na kisha kulazimishwa kushiriki katika ubakaji wa genge akiwa na umri wa miaka 14.

Soma pia: Madai ya ubakaji dhidi ya TB Joshua yawatikisa Wanjilisti wa Afrika

Pélicot pia alizungumza juu ya kiwewe alichopitia wakati wazazi wake walipomchukua msichana mdogo katika familia, na kushuhudia tabia isiyofaa kutoka kwa baba yake. "Baba yangu alikuwa akifanya vivyo hivyo na msichana huyo mdogo," alisema.

Mamia ya watu wamekusanyika katika maandamano kote Ufaransa kuonyesha mshikamano na Gisele Pelicot.Picha: Abdul Saboor/REUTERS

"Baada ya kifo cha baba yangu, kaka yangu alisema kuwa wanaume walikuwa wakija nyumbani kwetu." Katika umri wa miaka 14, alisema, alimuuliza mama yake kama angeweza kuondoka nyumbani, lakini "hakuniruhusu."

"Sitaki kabisa kuzungumza juu ya hili, ninamuonea aibu tu baba yangu. Mwishowe, sikufanya vizuri zaidi," alisema Pélicot kuhusu hisia zake kwa mke wake, alisema hakustahili alichokifanya.

"Tangu ujana wangu, nakumbuka mishtuko na kiwewe tu, niliyasahau tu kwa msaada wake. Hakustahili hii, nakubali," alisema huku akitokwa na machozi.

Wakati huo, Gisèle Pélicot, akiwa amesimama kando ya chumba hicho, akimtazama mbele ya kundi la washtakiwa kadhaa aliokuwa ameketi katikati yao, anavaa tena miwani yake ya jua.

Baadaye, Dominique Pélicot alisema, "Nilikuwa na wazimu juu yake. Alibadilisha kila kitu. Niliharibu kila kitu."

Afisa usalama alimnasa Pélicot mnamo 2020 akirekodi video chini ya sketi za wanawake kwenye duka kubwa, kulingana na nyaraka za mahakama.

Polisi walipekua nyumba ya Pélicot na vifaa vya elektroniki, na kupata maelfu ya picha na video za wanaume wakifanya mapenzi na Gisèle Pélicot huku akionekana amelala bila fahamu kwenye kitanda chao. Kwa rekodi hizo, polisi waliweza kuwasaka washukiwa wengi 72 waliokuwa wakiwatafuta.

Maandamano ya kumuunga mkono Gisele Pelicot na waathiriwa wote wa ubakaji, huko Bordeaux, Ufaransa mnamo Septemba 14, 2024.Picha: Patrice Pierrot/abaca/picture alliance

Washangazwa na usiri wa miaka 50

Gisèle Pélicot na mume wake walioishi naye kwa miaka 50 walikuwa na watoto watatu. Walipostaafu, wenzi hao waliondoka katika mkoa wa Paris na kuhamia katika nyumba moja huko Mazan, mji mdogo uliko mkoa wa Provence.

Soma pia: Tanzania: Polisi anayehusishwa na ubakaji afikishwa kortini

Wakati maafisa wa polisi walipomwita kumhoji mwishoni mwa 2020, awali aliwaambia mumewe alikuwa "mtu mzuri," kulingana na nyaraka za kisheria. Kisha wakamwonyesha baadhi ya picha. Alimuacha mumewe na sasa wametalakiana.

Anakabiliwa na kifungo cha miaka 20 jela iwapo atapatikana na hatia. Kando na Pélicot, wanaume wengine 50, wenye umri wa miaka 26 hadi 74, wanashtakiwa mahakamani.

Bernadette Tessonière, mstaafu mwenye umri wa miaka 69 ambaye anaishi mwendo wa nusu saa kwa gari kutoka Avignon, ambako kesi hiyo inasikilizwa, alifika nje ya mahakama saa moja na robo asubuhi ili kuhakikisha kuwa atapata kiti katika kesi hiyo inayofuatiliwa kwa karibu.

"Inawezekanaje kwamba katika miaka 50 ya maisha ya kijamii, mtu anaweza kuishi karibu na mtu ambaye anaficha maisha yake vizuri? Hii inatisha," alisema, akiwa amesimama kwenye mstari nje ya mahakama.

 "Sina matumaini makubwa kwamba alichofanya kinaweza kuelezewa, lakini angalau atatoa vipengele kadhaa."

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW