1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwandishi aliyekimbia mateso Uganda awasili Ujerumani

23 Februari 2022

Mwandishi maarufu wa Uganda Kakwenza Rukirabashaija aliyekimbia nchi baada ya kushtakiwa kwa kumtusi Rais Yoweri Museveni na mwanawe, amewasili Ujerumani kwa matibabu baada ya kuteswa gerezani.

Uganda Autor Kakwenza Rukirabashaija
Picha: ABUBAKER LUBOWA/REUTERS

Wakili wake Eron Kiiza ameliambia shirika la habari la AFP kuwa mwandishi huyo amewasili Ujerumani asubuhi ya Jumatano na kuielezea habari hiyo kama afueni kubwa.

Mwandishi huyo alizuiliwa muda mfupi baada ya sherehe za Krismasi na baadaye kushtakiwa kwa kufanya "mawasiliano ya kukera" katika kesi ambayo ilizua wasiwasi wa kimataifa.

Umoja wa Ulaya ulikuwa miongoni mwa waliotoa wito wa kufanyika uchunguzi wa kina kuhusu ukiukwaji wa haki nchini Uganda. Rukirabashaija, mwenye umri wa miaka 33, alitoroka Uganda wiki mbili zilizopita baada ya mahakama kukataa ombi lake la kurejeshewa pasipoti yake na kabla ya kesi ya jinai ambayo ingelitakiwa kuanza leo.

Alisema aliteswa akiwa kizuizini na alionekana kwenye runinga mapema mwezi huu na kufichua makovu yaliyokuwa yakionekana kutapakaa mgongoni mwake na kwenye sehemu nyengine za mwili wake.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW