1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwandishi habari maarufu wa Zimbabwe akamatwa

10 Januari 2021

Hopewell Chin’ono aliandika ujumbe twita akisema polisi wamemuua mtoto mchanga wakati wakitekeleza sheria za kuzuia kusambaa virusi vya Corona imemponza mwandishi huyo wa habari ambaye ni mkosoaji wa rais Mnangagwa

Simbabwe Hopewell Chin’ono
Picha: Getty Images/AFP/J. Nijikizana

Mwandishi habari mashuhuri nchini Zimbabwe aliyeshtakiwa kwa kuandika habari za uwongo amepelekwa jela na kutengwa katika chumba cha peke yake baada ya kugundulika  huenda alikutana na watu wenye maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 kabla ya kukamatwa kwake. Siku ya ijumaa polisi wa Zimbabwe walimkamata Hopewell Chin'ono kwa mara ya tatu katika kipindi cha miezi mitano.

Hatua hiyo ya kukamatwa hivi sasa imekuja baada ya mwandishi huyo wa habari kuandika ujumbe wa Twitta akidai kwamba polisi walimpiga mtoto mchanga mpaka akafariki wakati wakitekeleza hatua ya kusimamia utaratibu wa kuzuia kusambaa ugonjwa wa Covid-19 nchini humo wiki hii.

Hata hivyo polisi ilisema kwamba taarifa hizo ni za uwongo. Siku ya Jumamosi mawakili wa mwandishi habari huyo walipambana kudai uhuru wa mteja wao wakisema kwamba kukamatwa kwake ni hatua iliyochukuliwa kinyume cha sheria lakini mahakama haikuweza kumaliza kusikiliza hoja za utetezi na badala yake wakamsweka rumande.

Picha: Getty Images/AFP/J. Nijikizana

Wakili wake Harrison Nkomo amesema Chin'ono huenda alikutana na watu walioambukizwa virusi vya Corona wakati alipoitembelea Afrika Kusini hivi karibuni ,sababu ambayo wanadai ndiyo inayopaswa kuangaliwa kumuachia huru aruhusiwe kukaa nyumbani.

Kwa upande mwingine upande wa mashtaka umesema kukutana kwake na waliombukizwa virusi hivyo ndiyo sababu ya kumfanya apelekwe rumande ili kuepusha kusambaza virusi hivyo hadi pale atakapofanyiwa uchunguzi wa kimatibabu.

Jaji Lazini Ncube alitoa agizo,kwamba  mwandishi habari huyo apelekwe jela na kuwekwa katika chumba cha  peke yake wakati ombi lake la kutaka aachiwe huru likipangwa kuendelea kusikilizwa siku ya Jumatatu.

Picha: Zinyange Auntony/AFP

Ikumbukwe kwamba mwandishi habari huyo kabla ya kukamatwa hivi sasa,alikuwa ameachiwa huru kwa dhamana kutokana na tuhuma za kuhusika na uchochezi baada ya kuyaunga mkono maandamano ya kuipinga serikali mnamo mwezi Julai pamoja na kudaiwa kuipaka tope idara ya uendeshaji mashtaka ya Zimbabwe kwa kudai kwamba rushwa imetapakaa ndani ya chombo hicho.

Chin'ono ni mmoja wa waandishi habari maarufu sana nchini Zimbabwe anayefahamika kuwa mkosoaji wa serikali ya rais Emmerson Mnangagwa akiishutumu kwa ufisadi na ukiukaji wa haki za binadamu. Hata hivyo serikali ya Zimbabwe inazipinga  tuhuma hizo.

Kabla ya kukamatwa mwezi Julai Chin'ono alichapisha kwenye mtandao wa Twitta taarifa ya kufichua madai ya rushwa yaliyohusisha matumizi ya dola milioni 60 kuwanunulia vifaa vya kujikinga wafanyakazi wa huduma ya afya. Baada ya tuhuma hizo rais Mnangagwa baadae alimfuta kazi waziri wa afya ambaye alifunguliwa rasmi mashtaka ya rushwa.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Saumu Njama

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW