Mwanzo wa mwisho wa Ntaganda wawadia?
19 Machi 2013Ntaganda aliingia katika ubalozi wa Marekani mjini Kigali jana Jumatatu, na kuomba asafirishwe hadi mjini The Hague, ilipo mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita, ambako anakabiliwa na mashtaka ya uhalifu wa kivita wakati wa miaka kadhaa ya uasi.
Mwisho wa safari ndefu
Kwa kujisalimisha mjini Kigali, ambako afisa mmoja wa ubalozi alisema wafanyakazi walistushwa na kuwasili kwake kwa ghafla, Ntaganda amehitimisha safari ndefu iliyomshuhudia akipigana kama muasi na mwanajeshi wa serikali kwa pande mbili za mpaka wa Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, wakati wa mgogoro wa karibu miaka 20 katika kanda ya maziwa makuu.
Uwepo wa Ntaganda ulikuwa haujulikani baada ya mamia ya wapiganaji wake kukimbilia nchini Rwanda na wengine kujisalimisha kwa Umoja wa Mataifa mwishoni mwa wiki, kufuatia kushindwa kwake na kundi hasimu la M23 walilojitenga nalo. Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani, Victoria Nuland, alisema Ntaganda alitoa ombi makhsusi la kupelekwa katika mahakama ya ICC.
"Naweza kuthibitisha kuwa Ntaganda aliwasili katika ubalozi wa Marekani mjini Kigali na aliomba apelekwe ICC mjini The Hague. Kwa sasa tunawasiliana na serikali kadhaa ikiwemo ya Rwanda, ili kufanikisha maombi yake", Nuland aliwaambia waandishi wa habari mjini Washington.
Msemaji wa ICC Fadi El-Abdullah alisema mahakama hiyo itachukua hatua zote zinazohitajika kuhakikisha kuwa mtuhumiwa huyo anafikishwa haraka mjini The Hague, na kuongeza kuwa hakuna kizuizi kwa taifa lisilo mwanachama wa mahakama hiyo kushikirikiana nayo kwa msingi wa kujitolea. Rwanda na Marekani zote siyo wanachama wa ICC na kwa hivyo haziwajibiki kumkabidhi Ntaganda, lakini Nulanda alisema nchi yake inaunga mkono kupelekwa kwake huko.
Mashtaka yanayomkabili
Ntaganda anakabiliwa na mashtaka ya kuwatumikisha watoto vitani, mauaji, unyanyasaji wa kikabila, kuwatumikisha wanawake kingono na ubakaji wakati wa mgogoro wa mwaka 2002 hadi 2003, katika wilaya ya Ituri, kaskazini-mashariki mwa Kongo.
Lakini kwa mujibu wa wataalamu wa Umoja wa Mataifa, Ntaganda ambaye alipewa jina la "Terminator" alikuwa hivi karibuni, kiongozi wa waasi wa M23 walioendesha vita vya karibu mwaka mzima, na kuiadhiri serikali mjini Kinshasa na vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa, kwa kuuteka mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kaskazini Goma, mwezi Novemba mwaka jana. Wataalamu hao wanasema vita hivyo viliungwa mkono na Rwanda na Uganda, ambazo hata hivyo zinakanusha kupeleka majeshi yake kuwasaidia waasi hao.
Ntaganda ni nani hasa?
Ntaganda ambaye ni mzaliwa wa Rwanda, alikulia nchini Kongo kabla ya kupigana upande wa waasi wa Kitutsi walioiteka Rwanda na kukomesha mauaji ya halaiki ya mwaka 1994 ambamo zaidi ya watu 800,000 waliuawa. Baadae alirejea nchini Kongo ambako alishiriki katika mfululizo wa uasi, lakini pia alihudumu kwa muda kama Jenerali mwandamizi na alijijengea jina kwa biashara ya magendo ya madini.
Msemaji wa serikali ya Kongo Lambert Mende alisema Ntaganda alivuka mpaka na kuingia nchini Rwanda siku ya Kumamosi kwa msaada wa jeshi la Rwanda. Lakini waziri wa mambo ya nje wa Rwanda Louise Mushikiwabo alikanusha madai ya Kinshasa siku ya Jumapili, kuwa Ntaganda aliingia nchini humo, lakini alisema wapiganaji 600 kutoka kundi la M23 walikuwa wamevuka mpaka, akiwemo kiongozi wa zamani wa kisiasa Jean-Marie Runiga.
Alipoulizwa iwapo Rwanda itasaidia kuhamishwa kwa Rwanda mjini The Hague, waziri Mushikiwabo alisema nchi yake haihusiki kwa vyovyote na uamuzi huo kwa kuwa Ntaganda alikuwa katika eneo la Marekani.
Muda mfupi baada ya kuteuliwa kuwa mjumbe maalumu wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa katika kanda ya maziwa makuu, Mary Robinson alitowa wito siku ya Jumatatu kwa mataifa kushirikiana na ICC.
Aacha alama zisizofutika Kongo
Kushindwa kwa Ntaganda na kamanda mwingine wa waasi Sultan Makenga siku ya Jumamosi kulikuja baada ya wiki kadhaa za msuguano ndani ya M23, kundi la waasi la hivi karibuni kuongozwa na watutsi dhidi ya serikali ya mbali. Uasi wa M23 katika mkoa wa Kivu Kaskazini wenye utajiri mkubwa wa madini, ulisababishwa na mipango ya rais Joseph Kabila kumkata Ntaganda na kumkabidhi kwa ICC.
ICC ilitoa waranti wa kukamatwa kwa Ntaganda mwaka 2006, lakini rais Joseph Kabila alisita kuchukua hatua hadi Aprili mwaka jana, akisema Ntaganda alikuwa na nafasi muhimu katika kuendeleza amani nchini humo. "Kwa miaka 10 sasa, Ntaganda ameacha alama za ukatili mashariki mwa Kongo, akiyaongoza majeshi yake kuua, kubaka, na kuteka nyara," alisema Ida Sawyer, mtafiti kutoka shirika la haki za binaadamu la Human Rights Watch na kuongeza kuwa Marekani inapaswa kuhakikisha anakumbana na mkono wa sheria kwa uhalifu huo, kwa kumpeleka mara moja ICC.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afpe,rtre
Mhariri: Josephat Charo