1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwendesha mashitaka wa Misri ajiuzulu

18 Desemba 2012

Katika tukio jingine linalofanya mzozo wa Misri kutokota hata zaidi, mwendesha mashtaka mkuu nchini humo, aliyeteuliwa hivi karibuni, Talaat Ibrahim Abdullah amejiuzulu wadhifa huo.

Präsident Mohammed Mursi mit neuem Generalstaatsanwalt Talaat Ibrahim
Ägypten Präsident Mursi mit dem ehemaligen Generalstaatsanwalt Talaat IbrahimPicha: picture-alliance/Photoshot

Mamia ya waendesha mashtaka ya umma walifanya mgomo nje ya ofisi ya Abdullah mjini Cairo wakimtaka ajiuzulu. Aidha wanamtaka Waziri wa Sheria Ahmed Mekki afutwe kazi. Hatua ya Rais Mohamed Mursi kumfuta kazi aliyekuwa mwendesha mkuu wa mashitaka Abdel Maguid Mahmoud mnamo mwezi Novemba ilichochea shutuma kutoka idara ya mahakama iliyodai kuwa uhuru wake unakandamizwa.

Kujiuzulu kwa Ibrahim kunatarajiwa kuwasilishwa mbele ya Baraza Kuu la Mahakama Jumapili ijayo. Kuhusu suala la madai ya udanganyifu katika uchaguzi huo wa Jumapili, Jaji Mohammed El-Tamboli, ambaye ni mwanachama wa Tume Kuu ya Uchaguzi amesema tume hiyo ilipokea malalamishi kutoka kwa wapiga kura wote na makundi ya kijamii kuhusu uwezekano wa kuwepo hila za udanganyifu. Matokeo ya uchunguzi huo yatatangazwa pamoja na matokeo ya mwisho ya kura ya maoni, yanayotarajiwa kutolewa baada ya duru ya pili ya upigaji kura Desemba 22.

Wafuasi wa Mursi wanadai kupata ushindi katika duru ya kwanzaPicha: Reuters

Upinzani nchini Misri unapanga kuongoza maandamano makubwa hii leo kulalamikia madai ya kuwepo udanganyifu katika duru ya kwanza ya kura ya maoni kuhusu katiba mpya iliyofanyika mwishoni mwa wiki.

Uchunguzi waendelea

Waislamu wenye itikadi kali wanaomuunga mkono rais Mohamed Mursi wanadai kupata ushindi katika kura hiyo. Maafisa nchini Misri wanaendelea na uchunguzi kuhusu madai ya udanganyifu katika duru ya kwanza ya kura ya maoni kuhusu katiba mpya wakati upinzani ukiitisha maandaamno ya kitaifa ya kuipinga katiba hiyo mpya iliyowasilishwa na rais Mohamed Mursi na wafuasi wake wa siasa kali za kiislamu.

Maandamano makubwa yanatarajiwa nchini MisriPicha: REUTERS

Matokeo ambayo hayajathibitishwa yameonyesha kwamba wapiga kura wengi katika mikoa kumi walioshiriki katika duru ya kwanza ya upigaji kura wameunga mkono katiba mpya. Makundi ya upinzani yameitisha maandamano ya kitaifa leo dhidi ya kura hiyo ya maoni. Upinzani unasema Katiba hiyo iliyoandikwa na bunge lililojaa waislamu wengi wenye itikadi kali, inaweza kuhujumu haki za wanawake na za kisiasa, pamoja na kuyatenga makundi ya walio wachache.

Wakati huo huo, wanaharakati wanne wanaofanya mgomo karibu na kasri la rais mjini Cairo wametangaza kwamba wanaanza mgomo wa kususia kula chakula katika jaribio la kumshinikiza Mursi kuondoka madarakani. Kama katiba mpya itaidhinishwa, Mursi ataitisha uchaguzi mpya wa bunge. Baraza la Shura au Senate, litapewa mamlaka ya kutunga sheria hadi pale bunge jipya litakapoundwa. Kama rasimu hiyo ya katiba itaangushwa, Mursi ataitisha uchaguzi katika kipindi cha miezi mitatu kulichaguwa bunge litakaloandika katiba mpya.

Mwandishi: Bruce Amani/DPA

Mhariri: Daniel Gakuba