1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwendesha mashtaka mpya wa ICC aapa kuifufua mahakama hiyo

Zainab Aziz Mhariri: Josephat Charo
16 Juni 2021

Mwanasheria wa Uingereza Karim Khan ameapishwa kuwa Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya kimataifa ya mjini The Hague ICC. Bwana Khan ameahidi kushirikiana pia na nchi ambazo si  wanachama wa mahakama hiyo. 

Bildkombo Internationaler Strafgerichtshof Fatou Bensouda und Nachfolger Karim Khan

Mwanasheria huyo mwenye umri wa miaka 51 anachukua wadhifa huo baada ya kumalizika muhula wa miaka 9 wa Fatou Bensouda kutoka Gambia. Karim Khan amesema atajaribu kuwezesha kesi kufanyika kwenye nchi ambako uhalifu unatendeka. Mwingereza huyo ana tajiriba ya miaka mingi kama mwanasheria wa kimataifa, mwendesha mashtaka na wakili. Amesema kipaumbele kwake ni katika kuhakikisha utekelezaji wa msingi wa mkataba uliowezesha kuundwa mahakama ya kimataifa, ICC na kuhakikisha kwamba mahakama hiyo inafuatilia uwajibikaji na kuhakikisha wanaotenda uhalifu wanaadhibiwa.

Karim Khan Mwendesha mashatka Mkuu mpya wa ICCPicha: Reuters

Mwendesha mashtaka huyo mpya bwana Khan anaanza kuutumikia wadhifa huo kwa kurithi mlima wa mafaili ulioachwa na jaji aliyemtangulia,Fatou Bensouda aliyejaribu kuyatandaza mamlaka ya mahakama ya ICC kiasi cha kugongana na Marekani iliyoamua kumwekea vikwazo. Kabla ya kuondoka Bensouda alisema alifanya maamuzi kwa makini bila ya woga au upendeleo. Karim Khan atakumbana na milundiko ya malalamiko yanayohusu Palestina, Afghanistan na Myanmar miongoni mwa mengine mengi.

Shirika la kutetea haki za binadamu duniani, Amnesty International limesema uteuzi wa bwana Khan ni fursa ya kurejesha nguvu za mahakama ya kimataifa ya mjini  the Hague. 

Mwendesha mashtaka mkuu huyo mpya bwana Khan ameeleza kuwa makao makuu ya mahakama ya mjini The Hague inapaswa kuwa korti ya mamlaka ya juu kabisa na kwamba pale inapowezekana kesi zifanyike kwenye nchi ambako uhalifu unafanyika. Khan pia amesisitiza umuhimu wa kushirikiana pia na nchi ambazo si wanachama wa mahakama ya ICC.

Mataifa makubwa ya Marekani, China na Urusi haziutambui mkataba wa Roma ambao ni msingi wa kuanzishwa kwa mahakama hiyo. Karim Khan ameelezea matumaini juu ya kuweza kupatikana msingi wa pamoja na nchi hizo katika juhudi za kuzuia mauaji ya halaiki, uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita.

Aliyekuwa rais wa Liberia Charles Taylor,aliyekuwa mmoja kati ya watu waliowakilishwa na Amir KhanPicha: AP

Hivi karibuni bwana Karim Khan aliongoza ujumbe wa Umoja wa Mataifa katika kuchunguza vitendo vya kikatili nchini Iraq na aliliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba alibainisha ushahidi dhahiri wa mauaji ya kimbari ya Wayazidi yaliyofanywa na magaidi wanaojiita dola la kiislamu mnamo mwaka 2014.

Mnamo miaka ya nyuma Karim Khan aliwatetea wateja kadhaa mashuhuri kwenye mahakama za kimataifa, ikiwa pamoja na aliyekuwa rais wa Liberia Charles Taylor, Naibu Rais wa Kenya William Ruto na Seif al- Islam, mtoto wa aliyekuwa rais wa Libya Muammar Gaddafi aliyeuawa baada ya kung'olewa madarakani.

Vyanzo:AP/AFP