Mwenge wa Olimpiki wawasili London
20 Julai 2012Mwenge huo ulibebwa ndani ya helikopta ya kijeshi na kuwekwa katika mnara wa London, mahali ambako Malkia anaweka vito vya thamani. Kuwasili kwa mwenge huo kunaongeza msisimko uliopo kabla ya kuanza mashindano hayo maarufu ulimwenguni.
Maandalizi ya michezo hiyo yamegubikwa na hofu ya usalama baada ya shirika lililoahidi kutoka walinzi wa kibinafsi kusema halingweza kutimiza ahadi hiyo ya kutoa walinzi 10,000.
Lakini mkuu wa michezo ya London 2012, Sebastian Coe, anasisitiza kuwa usalama hautahujumiwa, kwa sababu serikali imewasajili wanajeshi zaidi 3,500 kuziba upungufu uliokuwepo wa kampuni ya G4S, na walinzi wengine 2,000 wakiwekwa chonjo katika hali ya tahadhari.
Kemboi arejea nyumbani kwa mazoezi
Kutokana na kuchoshwa na mvua inayonyesha Uingereza, Bingwa wa zamani wa Olimpiki na bingwa mara mbili ulimwenguni katika mbio za mita 3,000, Mkenya Ezekiel Kemboi, ameamua kurejea nyumbani baada ya wiki moja ya mazoezi ya kabla ya Olimpiki mjini Bristol.
Kemboi ambaye anakabiliwa kesi mahakamani kuhusu madai ya kumdunga kisu mwanamke mjini Eldoret, alikuwa amejiunga na kikundi cha kwanza cha Olimpiki ambacho kimepiga kambi mjini Bristol, Kusini Magharibi ya Uingereza.
Alisema Bristol ni mji mzuri kwa mazoezi ya wanariadha wa masafa ya kadri na marefu na pia kunayesha mvua nyingi jambo ambalo siyo zuri kwake.
Uamuzi wake wa kurudi mjini Nairobi ambao una joto kiasi unaongeza uzito kwa msimamo uliochukuliwa na wanariadha wengi nyota waliokataa kufanyia mazoezi yao mjini Bristol, wakisema ni eneo la nyanda za chini, ikizingatiwa na nyanda za juu nchini Kenya, jambo wanalosema litasaidia maandalizi yao ya Olimpiki.
Semenya kuongoza ujumbe wa Afrika Kusini
Caster Semenya ataibeba bendera ya Afrika Kusini wakati wa Olimpiki. Semenya mwenye umri wa miaka 21, alisema ni heshima kwake kufanya alichokiita kuwa ni kitu kikubwa kama hicho na kubeba bendera ya taifa kwa niaba ya timu itakayoiwakilisha Afrika Kusini.
Hii itakuwa mara ya kwanza kwa Semenya kushindana katika Olimpiki. Miaka mitatu iliyopita alikumbwa na tetesi za utata wa jinsia yake kufuatiwa na ushindi wake mkubwa mjini Berlin, Ujerumani. Semenya alilalamika kuwa kutakiwa athibitishe yeye ni wa jinsia gani sio muhimu na kuwa itakuwa uvamizi wa faragha yake.
Alitengwa kwa miezi 11 wakati shirika la IAAF lilikuwa likihakiki majaribio ya jinsia yake na kukubaliwa kurudi katika mashindano mwaka 2010, lakini hangeweza kushindana kwa sababu ya maumivu ya mgongo. Mwaka uliopita alimaliza wa pili katika mbio za mita 800 kule Korea Kusini, licha ya kuhangaika na maumivu hayo.
Aidha, Semenya aliwaambia waandishi wa habari wa Ulaya kuwa jinamizi hilo ameliacha nyuma na kuwa ana matarajio ya kushinda dhahabu katika Olimpiki ambayo akipata atamtunukia Nelson Mandela ambaye ni mwanasiasa maarufu wa Afrika kusini.
Semenya, ambaye rekodi yake ya muda mfupi zaidi ni dakika 1.59 na sekunde 18, amewahi kushindwa mara 5 na mshindi wa Olimpiki ya mwaka 2008 na Mkenya Pamela Jelimo.
Mwandishi: Bruce Aman/DPA/Reuters/AP
Mhariri: Miraji Othman