Mwenyekiti wa kampuni la Siemens atiwa ndani
28 Machi 2007
Tuanze lakini na kasheshe ya Siemens.Gazeti la HANDELSBLATT linaandika:
„Kuanzia jana,kampuni la SIEMENS linajikuta likizongwa kweli kweli na kashfa-tangu jana hali ya mambo katika kampuni hilo kubwa la kiufundi imezidi kuharibika.Mwenyekiti wa kamati kuu ya kampuni hilo,JOHANNES FELDMAYER,ametiwa ndani.Jibu la suala watu wanalojiuliza,kama kweli yote haya yanayofichuliwa hadharani tangu miezi kadhaa sasa ni kweli au la, linazidi kujitokeza:hadaa na udanganyifu katika malipo ya simu,akaunti za benki za watumishi wasiojulikana wa ujenzi wa vinu vya umeme-hongo kwa mashirika kadhaa ya wafanyakazi ili waunge mkono madai ya waajiri,mradi yadhihirika kana kwamba si dhana tena sasa kwamba uongozi wa Siemens hauchelei ikilazimika kutumia fedha ili kulifikia lengo lao.“
Hata gazeti la ABENDZEITUNG la mjini München linahisi kashfa hii ya sasa ya Siemen imechukua sura mpya kabisa.Gazeti linaandika:
„Kwamba kampuni linajaribu kuwashawishi wanaharakati wa mabaraza ya wafanyakazi-si jambo jipya-kama tulivyojionea katika kashfa ya kampuni la Volks-Wagen.Katika kampuni la SIEMENS mambo yamechukua kipeo kipya kabisa.Kwanza-kwasababu kwa mara ya kwanza tangu kuzuka kashfa za fedha za hadaa,mkuu wa Siemens ametiwa pingu.Pili kwasababu katika kampuni la Siemens suala halihusu pekee ziara za anasa na kutembelea madanguro.Ikiwa tuhuma za mwendesha mashtaka ni kweli,basi mwenyekiti wa kamati kuu ya Siemens atakua kweli ametoa mamilioni ya fedha kununua kura za wakuu wa mashirika ya waajiriwa.Kwa namna hiyo hoja za viongozi wa Siemen eti wanafuata maadili ya kikazi ni dhihaka tuu.!“
Mada ya pili ni kuhusu uchunguzi kama mtoto kweli ni wa baba yule anaedhaniwa.Mnamo siku zijazo akinababa hawatakua na kazi ngumu upande huo na wala hakutakua na madhara ya kisheria kwa watoto.Waziri wa sheria wa serikali kuu ya Ujerumani Brigitte Zypries ametunga mswaada wa sheria kwaajili hiyo.Gazeti la mjini Mainz-ALLGEMEINE ZEITUNG linaandika:
„Maendeleo makubwa,mtu anaweza kusema ni hatua ya kimapinduzi hii inayohusu sheria za familia-hasa katika suala la kutaka kujua kama mtoto ni wa baba au la.Mswaada huo wa sheria unarahisisha mambo na kuepusha mivutano isiyokua na maana.Baba ataendelea kuitumia haki yake ya kutaka kujua ukweli ukoje-halazimiki,kupitia mahakamani ili kuipata haki hiyo.Na hata ikidhihirika kwamba mtoto pengine si wake-mafungamano yao hayatavunjika.
Gazeti la STUTTGARTER NACHRICHTEN linahisi si mengi yatakayobadilika:
„Baba ataendelea tuu kisiri siri kuchunguza kama kweli mtoto ni wake.Kwanza,kwasababu amani ya familia itachafuka vibaya sana akilazimika kulifikisha suala hilo mahakamani.Na pili kwasababu uchunguzi wa kisiri siri,japo kama si halali-lakini anaechagua njia hiyo hana hatia pia.Zypries anataka kupiga marufuku uchunguzi wa kichini chini.Lakini suala hilo anaonelea bora kumuachia waziri wa afya Ulla Schmidt ambae tangu miaka kadhaa sasa anajaribu kutunga mswaada wa sheria kuhusu kutathiminiwa viini vya maumbile-DNA.“