Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika kuzuru Kenya wiki ijayo
6 Januari 2008Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, rais wa Ghana John Kufuor, atazuru Kenya wiki ijayo katika juhudi ya kuumaliza mzozo wa kisiasa na machafuko ya kikabila nchini humo.
Waziri wa mashauri ya kigeni wa Ghana, Akwasi Osei Adjei, amesema kwamba rais Mwai Kibaki amemualika rasmi rais John Kufuor kwenda Kenya kutathimini hali ilivyo na atoe ushauri kwa pande zinazozozana.
Rais Kufuor atazungumza na pande zinazohasimiana nchini Kenya kuhakikisha amani inadumishwa nchini humo. Hata hivyo haijulikani ni lini ziara ya mwenyekiti huyo wa Umoja wa Afrika itakapofanyika.
Tangazo hilo limetolewa baada ya naibu waziri wa mashauri ya kigeni wa Kenya, bwana Moses Wetangula, kufanya ziara rasmi nchini Ghana, ambako alikutana na waziri wa mambo ya kigeni wa nchi hiyo mjini Accra.