1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Mwezi wa damu" wasisimua watazamaji

Sekione Kitojo
28 Julai 2018

Kupatwa kwa muda mrefu zaidi kwa kile kilichojulikana kama "mwezi wa damu" katika karne hii kumewasisimua watu waliokuwa wakiangalia duniani kote jana Ijumaa (27.07.2018).

Mondfinsternis 2018 | Deutschland
Picha: Getty Images/M. Hangst

Tukio hilo liliingiliana  na  kukaribia sana kwa sayari ya Mars na dunia katika  muda  wa  miaka 15, tukio ambalo ni  la kusisimua  angani.

Wakati sayari ya  mwezi  ambayo huongozana  na  sayari  ya  dunia wakati  wote, ikipita  taratibu  angani, makundi ya  watu walikusanyika  duniani  kote  kuweza  kupata  kuona  tukio  hilo  la kipekee  ambalo  ni  nadra.

Mwezi ulivyoonekana katika anga ya Sao Paulo nchini BrazilPicha: Reuters/P. Whitaker

Mbali  na  ziwa Magadi, kilometa  100 kusini  magharibi  mwa  mji mkuu  wa  Kenya, Nairobi, jamii  ya  vijana  wa  Kimaasai waliangalia  kupatwa  huko kwa  kutumia  teleskopu yenye nguvu iliyotolewa  na familia  inayoishi  katika  sehemu  hiyo.

"Hadi leo nilidhani Mars, Jupiter na  sayari  nyingine ilikuwa ni fikira tu  za  wanasayansi," Purity Sailepo , mwenye  umri wa  miaka  16 aliliambia  shirika  la  habari  la  AFP.

Lakini  sasa  nimeiona  na  naweza  kuamini  na  nataka  kuwa mtaalamu  wa  mambo  ya  anga ili  kuwaeleza  watu  wengine." Tofauti  na  kupatwa  kwa  jua, watazamaji  hawakuhitaji  kukinga macho  yao  kwa  kutumia  miwani ili  kuweza  kutazama  tukio  hilo la  nadra kutokea. Kwa  karibu  nusu  ya  dunia, mwezi ulikuwa  kwa sehemu  fulani  ama  kwa  ukamilifu  katika  kivuli  cha  dunia kwa muda  wa  masaa  sita  na  dakika  14.

Kipindi  cha  kupatwa  kamili , kilichofahamika  kama "kupatwa kamili", wakati  mwezi  uliopoonekana  kuwa  na  giza  zaidi , kilikuwa kwa muda  wa  saa  moja  na  dakika 43.

Mwezi ulivyoonekana katika tukio la kupatwa kwa mwezi , Cairo nchini MisriPicha: Reuters/A. A. Dalsh

Wakati  huo  huo, sayari  ya  mars  ilionekana  karibu  na  mwezi katika  anga  la  usiku, ilionekana  wazi  kwa  macho. Watalaamu  wa anga  ambao  wanafanya  shughuli  hiyo  kwa mapenzi  yao  tu katika  kizio  cha  dunia  cha  kusini  walikuwa  katika  nafasi  nzuri ya  kutazama  tukio  hilo,hususan  kusini  mwa  Afrika , Australia, na Madagascar, licha  ya  kuwa  tukio  hilo  pia  lilionekana  katika mataifa  ya  Ulaya , kusini mwa  Asia  na  Amerika  ya  kusini.

Watu wengi watazama tukio hilo

Zaidi  ya  watu 2,000 ikiwa  ni  pamoja  na  watoto  wengi  wakiwa na  vifaa  vya  kuona  mbali  walijikusanya  katika  mji  mkuu  wa Tunisia , Tunis.

"Ninamatumaini  kwamba  kupatwa  huku  kutatuletea  furaha  na amani," amesema Karima, mwenye  umri  wa  miaka  46, bila  ya kuondoa  macho  yake  angani.

Mwezi ulivyoonekana wakati wa kupatwa kwa mwezi nchini Ujerumani Picha: Getty Images/M. Hangst

Hata  hivyo , hali  mbaya  ya  hewa  ilizuia kuonekana  kwa  hali  hiyo katika  sehemu  kadhaa  za  dunia. Mvua  kubwa  za  majira  ya monsuni  na  mawingu  mazito  vilizuwia  kuonekana  kwa  mwezi katika  eneo  kubwa  la  India  na  majirani  zake, maeneo  ambayo yalipaswa  kuwa  na  muonekano  mzuri. Hata  pia , watazamaji waliokuwa  na  shauku  ambao  walijikusanya   katika  vilima  na fukwe za  bahari  katika  kaunti ya  Uingereza  ya  Dorset walibaki gizani  kutokana  na  mawingu  mazito.Wale  waliojikusanya  katika mji  mkuu  wa  Brazil Rio de Janeiro walikuwa  na  bahati  zaidi, wakiuona  mwezi  huo  mwekundu  katika  anga  iliyokuwa  wazi wakiwa  na  simu  zao  na  kamera.

"Nafikiri  ilikuwa  nzuri  sana, na  niliipenda  sayari  ya  Mars  zaidi, ambayo  iliweza  kuonekana  karibu  kabisa  na  mwezi," amesema Talita Olivera , mwenye  umri  wa  miaka  34.

sayari  ya  Mars  ilionekana  kuwa  kubwa  kuliko  kawaida  na angavu  zaidi, ikiwa  kilometa  milioni  57.7 kutoka  sayari  ya  dunia katika mhimili  wake kuzunguka  dunia. Kupatwa  kamili  kwa  mwezi kunatokea  wakati  dunia ikiwa katikati  ya  mwezi  na  jua, na kuzuwia  mwanga  wa  moja  kwa  moja  kutoka  katika  jua  ambao kwa  kawaida hufanya  mwezi  kung'ara kwa  rangi  nyeupe iliyochanganyika  na  njano.

Ndege ikiruka wakati mwezi ukiwa umepatwa, kaskazini mashariki mwa ChinaPicha: picture-alliance/Imaginechina/S. Yipeng

Mwezi husafiri kwenda  katika  eneo  maalum  kila  mwezi , lakini muelemeo  wa  mzunguko  wake  una  maana  kwa  kawaida  unapita juu  au  chini  ya  kivuli  cha  dunia, kwa  hiyo miezi mingi  tunapata mwezi mpevu bila  ya  kupatwa.

Wakati sayari  hizo  tatu  zikiwa  katika  msitari  mmoja , hata  hivyo, hali  ya  hewa  ya  dunia  inasambaza  mwanga  wa  buluu  kutoka katika  jua  wakati  ikitoa  mwanga  mwekundu  katika  mwezi, na huupa  mwezi  rangi ya  hudhurungi.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / afpe

Mhariri: Lilian Mtono

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW