Mwili wa Odinga wawasili Kisumu tayari kuagwa na umati
18 Oktoba 2025
Umati mkubwa wa waombolezaji umekusanyika leo Jumamosi katika mji wa magharibi mwa Kenya, Kisumu ili kuaga mwili wa mwanasiasa mkongwe Raila Odinga. Maombolezo ya Odinga aliyefariki dunia Jumatano wiki hii, yamegubikwa na ghasia na kusababisha vifo vya watu watano mjini Nairobi kutokana na umati mkubwa wa watu uliojitokeza kumuaga.
Kulikuwa na dalili za kutokea ghasia tena wakati jeneza la mwili wake lilipokaribia uwanja wa Kisumu, huku kundi kubwa la waombolezaji likikiuka vizuizi vya usalama na kupanda kwenye kuta.
Vikosi vya usalama vililazimika kufyatua risasi siku ya Alhamis, ili kutawanya umati mkubwa katika uwanja wa michezo jijini Nairobi ambako mwili wa Odinga ulipelekwa kuagwa. Maombi ya kitaifa yalifanyika jana Ijumaa na kuongozwa na Rais wa Kenya William Ruto. Odinga atazikwa kesho Jumapili katika eneo la Bondo karibu na kaunti ya Siaya.