1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwimbaji maarufu Grönemeyer anailaumu siasa ya maendeleo ya Ujerumani

Nina Werkhäuser / Maja Dreyer11 Julai 2006

Kabla ya mkutano wa kilele wa nchi nane tajiri duniani zilizomo kwenye kundi la G8 utakaofanyika mjini St. Petersburg, Urusi kuanzia Jumamosi ijayo, mashirika yasiyo ya kiserikali yanaitaka serikali ya Ujerumani iongeze juhudi zake za kuupiga vita umaskini na magonjwa duniani. Masharika haya yanasaidiwa na wasanii maarufu wa Kijerumani, kama vile Herbert Grönemeyer.

Herbert Grönemeyer
Herbert GrönemeyerPicha: AP

Herbert Grönemeyer amechoshwa kusikia hotuba za wanasiasa zinazosikika kabla na baada ya mikutano ya nchi za G8. Kuahidi kupiga vita umaskini ndiyo sawa, anasema mwimbaji huyu, lakini muhimu zaidi ni kutekeleza ahadi hizo: “Baada ya mkutano uliopita wa nchi nane zinazoongoza kiviwandi duniano, G8 mjini Gleneagles huko Scotland mwaka jana tunadhani ahadi nyingi zilitolewa na huenda hatua fulani zimechukuliwa. Lakini kwa ujumla tunaamini kuna uwongo mwingi.”

Mfano mmoja wa kudanganya ni kwamba katika bajeti yake serikali ya Ujerumani iliandika kufutwa madeni ya Iraq na Nigeria kuwe kama msaada wa maendeleo. Hivyo ujumla wa msaada wa maendeleo ulikuwa mkubwa. Grönemeyer amesema: “Ni kitu cha ujanja! Serikali hailipi centi moja, lakini inabadilisha bajeti yake kwa kujumuisha kufutwa madeni.”

Serikali lakini inapinga kulaumiwa, ikisema njia hiyo ya kuhesabu msaada wa maendeleo inatumika pia na Shirika la ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo OECD. Hata hivyo, kwa mujibu wa Bw. Grönemeyer na zaidi ya mashirika 100 ya Kijerumani yasiyo ya Kiserikali, jitihada za serikali ya Ujerumani kupiga vita umaskini hazitoshi. Mfano mmoja ni ugonjwa wa ukimwi: Mpaka sasa kila mgonjwa wa tano tu anaweza kupata madawa ya kurefusha maisha yake.

Serikali ya Ujerumani inalaumiwa kutotoa mchango wa kutosha kwenye mfuko wa nchi za G8 kwa ajili ya miradi ya afya, anasema mwimbaji Herbert Grönemeyer: “Ujerumani iko nyuma kabisa, Uingereza na Ufaransa zinalipa zaidi. Kwa hivyo tunamtaka Kansela Angela Merkel kutotoa ahadi tu. Sifa yetu duniani ni kwamba Ujerumani itekeleze ahadi zake, lakini hadi sasa hiyo haijatokea.”

Suluhisho lakini siyo tu kuomba fedha zaidi kutoka kwa serikali ya Ujerumani bali pia kutafuta njia nyingine za kupata fedha. Huko Ufaransa kwa mfano kila abiria wa ndege analipa kiasi fulani cha karo kwa ajili ya kupiga vita ukimwi, Malaria au kifua kikuu.

Mwaka ujao Ujerumani itachukua uwenyekiti wa nchi za G8 pamoja na jukumu la kutayarisha mkutano kwenye kisiwa cha Rügen. Grönemeyer na wenzake wa mashirika yasiyo ya kiserikali tayari wanafikiria vipi watakavyoweza kuwakumbusha wanasiasa watekeleze ahadi zao kwa kelele kubwa.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW