1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwito wa Raîla kwa Kenyatta kuhusu uteuzi wa majaji

Shisia Wasilwa
14 Juni 2021

Raila Odinga amemtaka Rais Kenyatta kuwaelezea bayana Wakenya sababu za kukataa kuwateua majaji sita kama walivyopendekezwa na Tume ya Idara ya Mahakama.

Kenia Symbolbild Wahlen und Social Media
Picha: AFP/T. Karumba

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, Raila amesema kuwa taifa linahitaji kuwa na mjadala wa maana kuhusu uteuzi wa majaji hao badala ya kelele zinazosikika kutoka kwa makundi mbali mbali.

Kiongozi huyo ambaye ananyoshewa kidole cha lawama kwa kuyaacha yale aliyopigania alipokuwa katika upinzani, ameonekana akimtetea rais Uhuru Kenyatta ambaye amekuwa akikwaruzana na idara ya mahakama na hata kukiuka baadhi ya maamuzi ya mahakama.


''Huo ni unafiki mtupu''

Rais Kenyatta alikataa kuwateuwa majaji wa mahakama kuu ambao walipangiwa kupandishwa cheo.Picha: picture alliance/AP Photo

Raila alimkosoa Jaji Mkuu wa zamani Willy Mutunga aliyenukuliwa akisema kuwa ni kichekesho kwa rais Kenyatta kuwataka wakenya kuheshimu sheria ilhali mwenyewe anakiuka.

''Wakati wa uchaguzi wa mwaka 2013, tulienda mahajkamani tukapeleka ushahidi wote. lakini walisema ushahidi huo umechelewa. Nani aliyesema haya si mwingine ni Willy Mutunga. Baadaye umemuona maeanza kusema kuwa hakuna haki na kadhalika...Mwenyewe katunyima sisi haki aliipokuwa Jaji Mkuu. Huo ni unafiki mtupu.'',alisema Raila.

Juma lililopita, Rais Kenyatta alikataa kuwateua majaji wa mahakama kuu wakiwemo, Joel Ngugi, George Odunga, Aggrey Muchelule na Weldon Korir- ambao walikuwa wamepangiwa kupandishwa cheo kuhudumu katika Mahakama ya Rufaa. Hatua ambayo iliibua cheche kutoka kwa majaji wakuu watangulizi David Maraga na Willy Mutunga.

Shinikizo kutoka kwa Jaji Mkuu

Jaji mkuu wa Kenya Matrha Koome akiapishwa jijini Nairobi.Picha: PPS-presidential press service

Raila ameongeza kusema kuwa mikwaruzano kati ya mihilimi ya serikali ni kinyume na kanuni za katiba na kwamba zinamuumiza mwananchi wa kawaida. Jaji Mkuu mpya Maartha Koome aidha ameijitosa kwenye mjadala huo.

Kinyume na mtangulizi wake Jaji David Maraga, Jaji Koome amesema kuwa atatumia njia za kidiplomasia kuleta uwiano kati yake na mhimili wa rais.

''Kama Jaji Mkuu na mwenye kiti wa tume ya idara ya mahakama,ningependa kusema kuwa watu wote walioagizwa na tume ya idara ya mahakama na kama ilivyo agizwa na katiba lazima wateuliwe kama majaji''.

Rais Uhuru Kenyatta alianza kukwaruzana na Idara ya Mahakama pindi tu baada ya ushindi wake kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka 2017 kubatilishwa. Uamuzi huo, ulithibitisha uhuru wa idara hiyo, lakini ukaanzisha mgongano kati ya mhimili wa rais na idara hiyo. Rais alinukuliwa akisema kuwa atarejelea uamuzi huo.

Matendo ya baadaye ya rais baada ya uamuzi huo, yamedhihirisha kuwa amekuwa akiilenga idara hiyo. Ikiwa imesalia miezi 13 kabla ya rais Kenyatta kukamilisha mihula yake miwili ya utawala, mkwaruzano wake na Idara ya Mahakama huenda isitiwe kikomo hivi karibuni, baada ya mahakama kuamua kuwa Mpango wa Maridhiano wa taifa kuwa kinyume na katiba.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW