1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwongozo wa watu kuishi pamoja Ujerumani

Oumilkheir Hamidou
2 Mei 2017

Hoja za waziri wa mambo ya ndani Thomas de maizière kuhusu mwongozo wa watu kuishi pamoja nchini Ujerumani zinazidi kuzusha mjadala. Kama wana CDU/CSU wanaziunga mkono, SPD na upande wa upinzani wanazikosoa

Bild am Sonntag Innenminister Thomas de Maiziere
Picha: Bild/Foto: DW/M. Fürstenau

 

Lawama dhidi ya hoja za waziri wa mambo ya ndani wa serikali kuu ya Ujerumani Thomas de Maizière zimetolewa miongoni mwa wengineo na mgombea kiti cha kansela kutoka chama cha Social Democrats SPD, Martin Schulz anaesema: " Mwongozo wa watu kuishi pamoja nchini Ujerumani umetajwa ndani ya sheria msingi ya Ujerumani na kumaanisha Uhuru, haki na watu kuishi pamoja kwa wema" amesema mwenyekiti huyo wa chama cha SPD. Ameongeza kusema waziri de Maizière amezusha mjadala wa bure ili kuficha makosa yake mwenyewe.

Mwenyekiti wa kundi la chama cha siasa kali za mrengo wa kushoto katika bunge la shirikisho Bundestag, bibi Sahra Wagenknecht anasema, "Badala ya kupiga domo mara laki kuhusu mwongozo wa watu kuishi pamoja, waziri wa mambo ya ndani angefanya la maana kuhakikisha  kwamba maimam wanaotumwa na Erdogan hawasababishi mfarakano kutokana na hotuba zao za kueneza chuki misitikini."

"Mgeni asiyetaka kujumuika katika maisha ya kila siku Ujerumani ahame"

Mwongozo wa kuishi pamoja UjerumaniPicha: Bild/Foto: DW/M. Fürstenau

Waziri wa mambo ya ndani Thomas de Maizière amechapisha mpango wa vifungu kumi kupitia gazeti la Bild toleo la jumapili, kuhusu mwongozo wa watu kuishi pamoja nchini Ujerumani. Waziri de Maizière anasema anautathmini mwongozo huo kama "utaratibu wa watu kuishi pamoja." Kupitia lugha, katiba na kuheshimu sheria msingi na mengineyo kuna mambo yanayotufanya tuwe na mshikamano, yanayotufanya tuwe kama tulivyo na yanayotutafautisha na wengine," amesema Waziri wa Mambo ya Ndani wa serikali kuu ya Ujerumani.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa jimbo la Bavaria, Joachim Herrmann wa chama cha CSU, anatetea hoja za de Maizière, hata hivyo anataka zifuatiwe na vitendo: "Waziri wa Mambo ya Ndani ana haki anapohimiza umuhimu wa kutangulizwa mbele mwongozo wa watu kuishi pamoja nchini Ujerumani," ameliambia gazeti la Die Welt na kuongeza: "Hatuhitaji maneno matupu, tunataka yafuatwe kivitendo. Mgeni yeyote asiyetaka kujumuika katika maisha ya kila siku nchini Ujerumani, basi matokeo yake anabidi aihame nchi yetu," amesisitiza.

Wanawake waliovalia BurkhaPicha: DW/M. Brabant

"Jamii yetu ni ya uwazi, hatuna Burka"

Manfred Weber, naibu mwenyekiti wa chama cha CSU, ambae pia ni kiongozi wa kundi la wabunge wa kihafidhina katika bunge la Ulaya, anautaja mjadala kuhusu mwongozo wa watu kuishi pamoja kuwa "umepitwa na wakati." Katika ulimwengu ambapo uhamiaji ni changamoto kubwa, watu wanatafuta mwongozo," ameliambia gazeti la "Passauer Neue Presse". Mwongozo wa watu kuishi pamoja unazuwia mitindo ya jamii kuishi mbali mbali na kusaidia kufanikisha juhudi za kuishi pamoja watu wa tamaduni tofauti.

Katika mpango huo wa vifungu kumi, Thomas de Maizière amesifu miongoni mwa mengineyo desturi za Wajerumani kwa mfano "wanapojitaja majina yao, wanapopeana mikono kuamkiana, wanapoacha wazi nyuso zao. Jamii yetu ni ya uwazi, hatuna burka" amesema.

Mwandishi: Hamidou Oumilkheir/epd/AFP

Mhariri: Iddi Ssessanga

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW